Arsenal yakaribia kuwapa mikataba Saliba, Saka
Muktasari:
- Mikataba ya mastaa hawa inatarajiwa kumalizika 2027 na Arsenal inataka kuwasainisha dili mpya mapema kwa sababu kumekuwa na timu mbalimbali zinazohitaji huduma zao.
ARSENAL ipo katika hatua za mwisho kwenye mazungumzo yake ya kuwaongeza mikataba, Bukayo Saka na William Saliba, wenye umri wa miaka 24 kila mmoja.
Mikataba ya mastaa hawa inatarajiwa kumalizika 2027 na Arsenal inataka kuwasainisha dili mpya mapema kwa sababu kumekuwa na timu mbalimbali zinazohitaji huduma zao.
Saka na Saliba ni wachezaji tegemeo wa Arsenal. Saka tayari amefunga mabao matatu na kutoa pasi mbili za mabao kwa msimu huu, huku Saliba akiendelea kuwa nguzo ya safu ya ulinzi.
Mara kadhaa Real Madrid ya Hispania imekuwa ikitajwa sana kutaka kumsajili Saliba ingawa hadi sasa hakuna ofa yoyote iliyoripotiwa kuwasilishwa katika meza ya Arsenal.
Kwa upande wa Saka vigogo kama Madrid na Manchester City wamekuwa wakitajwa kutaka kumsajili na wakati huu ambapo mkataba wake unaelekea ukingoni presha imeendelea kuwa kubwa.
Elliot Anderson
MANCHESTER United inapanga kumsajili kiungo wa Nottingham Forest na England, Elliot Anderson, mwenye miaka 22, katika dirisha lijalo la majira ya baridi na tayari imeshaanza kufanya mazungumzo na wawakilishi wake. Anderson amekuwa mmoja wa viungo chipukizi wanaoibukia England. Msimu huu ameanza katika mechi 4 kati ya 6 za Ligi Kuu England akiwa na Forest, pia amekuwa akicheza katika timu ya vijana ya England.
Tyrell Malacia
BEKI wa kushoto wa Manchester United na Uholanzi, Tyrell Malacia, mwenye umri wa miaka 26, anaweza kutua kwa mkopo wa msimu mzima katika klabu ya Eyupspor ya Uturuki. Malacia amekuwa nje kwa muda mrefu kutokana na majeraha ambayo yamekuwa yakimwandama mara kwa mara.
Msimu uliopita alicheza mechi 21 za michuano yote. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu.
Aaron Bouwman
LIVERPOOL na Manchester United ni kati ya klabu zinazomfuatilia kwa karibu beki chipukizi wa Ajax, Aaron Bouwman, mwenye miaka 18, raia wa Uholanzi. Bouwman anatajwa kama “Virgil van Dijk mpya” kutokana na urefu wake pamoja na uwezo wa kudhibiti mipira ya juu. Amepandishwa kucheza kikosi cha wakubwa cha Ajax kwa msimu huu baada ya kupandishwa akitokea timu ya vijana.
Fabio Vieira
HAMBURG ya Ujerumani ina nafasi ya kumsajili moja kwa moja kiungo raia wa Ureno, Fabio Vieira, mwenye umri wa miaka 25, ambaye anawatumikia kwa mkopo.
Timu hiyo inaweza kumpata Vieira kwa dau la Euro 20 molioni. Vieira alijiunga na Arsenal akitokea Porto mwaka 2022 kwa takribani Euro 35 milioni lakini hakuwa anapata nafasi ya kutosha katika viunga hivyo.
Aymeric Laporte
BEKI wa zamani wa Man City, Aymeric Laporte, 31, bado anasubiri uamuzi wa FIFA kama itamruhusu kuichezea Athletic Bilbao aliyosaini mkataba wa kuitumikia akitokea Al-Nassr katika dirisha lililopita lakini dili lilifeli katika dakika za mwisho baada ya kutokamilika kwa baadhi ya nyaraka. Baada ya hali hiyo, Bilbao iliiandikia barua FIFA kuomba staa huyo aruhusiwe lakini hadi sasa kimya.
Casemiro
KIUNGO wa kimataifa wa Brazil, Casemiro, 33, ambaye awali alihusishwa na uhamisho kwenda Saudi Arabia, huenda Manchester United ikaendelea kuwa naye hadi mkataba wake utakapomalizika kwa sababu ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo na yupo katika mipango ya kocha Ruben Amorim.
Jonathan David
INTER Milan ilionyesha nia ya kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Canada, Jonathan David, 25, katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi kabla hajatua Juventus kwa usajili huru baada ya kumaliza mkataba wake na Lille mwisho wa msimu uliopita.
David alikuwa na msimu bora Lille 2023/24 akifunga mabao 19 ya Ligue 1 na msimu huu akiwa na Juventus amecheza mechi mbili na kufunga bao moja.