Arsenal yahamishia nguvu kwenye saini ya Sesko
Muktasari:
- Arsenal inahitaji straika mpya kwenye kikosi na hivyo wanamtazama mkali huyo wa kimataifa wa Slovania mwenye umri wa miaka 21 kama chaguo bora kutokana na kiwango chake na unafuu wake wa kupatikana kwa bei ndogo.
ARSENAL imeripotiwa kuhamishia nguvu zote kwenye usajili wa straika wa RB Leipzig, Benjamin Sesko kwa ajili ya kuimarisha kikosi chao kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.
Arsenal inahitaji straika mpya kwenye kikosi na hivyo wanamtazama mkali huyo wa kimataifa wa Slovania mwenye umri wa miaka 21 kama chaguo bora kutokana na kiwango chake na unafuu wake wa kupatikana kwa bei ndogo.
Miamba hiyo ya Emirates imekuwa na orodha ndefu ya washambuliaji inaowasaka, lakini inamtazama Sesko kuwa nafuu kwao ukilinganisha na mkali wa Newcastle United, Alexander Isak, ambaye ukiweka kando kutakiwa pia na Liverpool, bei yake anayouzwa ni kubwa.
Katika kuepuka kutumia pesa nyingi kwa mchezaji mmoja, ambaye kiwango chake unaweza kukipita kwa mchezaji mwingine, Arsenal imehamishia nguvu kwa Sesko ambaye amekuwa moto wa kuotea mbali huko kwenye Bundesliga.
ASTON Villa imeripotiwa kuingia kwenye vita na Arsenal katika mchakamchaka wa kufukuzia saini ya straika wa Serbia, Dusan Vlahovic, 25. Aston Villa inahitaji huduma ya mshambuliaji huyo baada ya kuwa na uhakika kwamba atakuwa tayari kuachana na Juventus mwishoni mwa msimu huu wakati wa uhamisho wa dirisha la majira ya kiangazi. Kwa muda mrefu, Vlahovic amekuwa akihusishwa na timu za England.
LIVERPOOL imeripotiwa kwamba ipo tayari kufungua milango kwa ajili ya kumpiga bei winga raia wa Colombia, Luis Diaz kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi. Kinachoelezwa ni kwamba Liverpool imelenga kupata Euro 70 milioni kwenye mauzo ya mshambuliaji huyo, ambapo klabu ya Atletico Madrid ya Hispania imeonyesha dhamira ya dhati ya kutaka huduma ya mchezaji huyo mwenye miaka 28.
KIPA, Robert Sanchez ameripotiwa kwamba hatafunguliwa mlango wa kutokea wakati wa dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Chelsea licha ya kuwa na kiwango duni na kuigharimu timu hiyo. Kulikuwa na ripoti kwamba Chelsea itaingia sokoni kusaka kipa mpya, lakini sasa Sanchez pamoja na Filip Jorgensen wataendelea kuaminika kwenye kikosi hicho.
BAYERN Munich imeripotiwa kuondoa ofa mezani kwa kiungo wa Kijerumani, Joshua Kimmich baada ya mchezaji huyo kusuasua kusaini dili jipya. Kutokana na hilo, Kimmich sasa ambaye mkataba wake utafika tamati mwishoni mwa msimu huu atakuwa huru kujiunga na timu yoyote bure kabisa. Timu kibao za Ligi Kuu England zimehusishwa na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 30.
KIUNGO wa Manchester United na Brazil, Casemiro, 33, ameripotiwa kuwekwa kwenye kundi muhimu AC Milan katika orodha ya wachezaji ambao watanaswa San Siro wakati wa dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi. Casemiro anaripotiwa kuwa mmoja wa wachezaji ambao Man United itafungua mlango wa kuachana nao mwishoni mwa msimu huu ili kunasa wakali wengine wapya.
ARSENAL imeripotiwa kwamba itakabiliana na upinzani mkali kutoka kwa AC Milan katika vita ya kusaka saini ya beki wa kushoto wa Wolves, Rayan Ait-Nouri. Mkali huyo wa Algeria mwenye umri wa miaka 23 amekuwa mmoja wa wachezaji wanaosakwa sana huko Ulaya kwa sasa kutokana na kiwango chake bora anachonyesha.
EVERTON imeripotiwa kufuta mpango wa kumchukua jumla winga wa Leeds United, Jack Harrison, 28, baada ya muda wake wa mkopo utakapofika tamati mwishoni mwa msimu huu. Awali kulikuwa na ripoti kwamba ingemchukua jumla, lakini baada ya kuona kiwango chake cha uwanjani, imefuta jambo hilo na kwamba Harrison atarudi zake Leeds.