Arsenal 'kufungia mlango' wanne

Muktasari:
- Vyanzo vya kuaminika vimeiambia tovuti ya The Mirror, tangu alipowasili mwezi Machi, Berta amekuwa akifanya kazi kwa bidii kuhakikisha anawabakiza wachezaji muhimu ndani ya timu msimu ujao.
LONDON, ENGLAND: MKURUGENZI wa michezo wa Arsenal, Andrea Berta anataka kuwasainisha mikataba mipya nyota wanne wa timu hiyo baada ya kuanza na beki Gabriel Magalhaes aliyeongeza hadi mwaka 2029.
Vyanzo vya kuaminika vimeiambia tovuti ya The Mirror, tangu alipowasili mwezi Machi, Berta amekuwa akifanya kazi kwa bidii kuhakikisha anawabakiza wachezaji muhimu ndani ya timu msimu ujao.
Bukayo Saka na William Saliba, ambao wana miaka miwili tu iliyosalia kwenye mikataba yao ya sasa, tayari wameanza mazungumzo na Arsenal kuhusu mikataba mipya na wameonyesha nia ya kuendelea kubaki. Awali kulikuwa na wasiwasi mastaa hawa wanaweza kuondoka lakini Saliba anayehusishwa na Real Madrid na Saka ambao ni sehemu muhimu ya kikosi cha Mikel Arteta, tayari wamezungumza hadharani kuhusu nia yao ya kuendelea kubaki Kaskazini mwa London.
Arsenal haina presha juu ya mchakato huo na inaelewa mazungumzo yanaweza kuchukua muda, lakini bado ina imani makubaliano yatafikiwa.
Wachezaji waliotoka katika akademi ya klabu hiyo Ethan Nwaneri na Myles Lewis-Skelly pia wanatarajiwa kusaini mikataba mipya ambayo pia itajumuisha nyongeza ya mishahara.
Mikataba yao ya sasa inatarajiwa kuisha dirisha lijalo la majira ya kiangazi mwaka 2026, lakini kuna matumaini makubaliano kwa wachezaji wote wawili yako karibu kufikiwa.
Mazungumzo na Lewis-Skelly yalianza kabla ya kuwasili kwa Berta, ambaye baada ya kuajiriwa kama mkurugenzi wa michezo wa Arsenal alianza kuwasiliana na wawakilishi wa Nwaneri kupendekeza mazungumzo rasmi ya mkataba, ambayo sasa yanaendelea.
Mazungumzo pia bado yanaendelea na Thomas Partey, ambaye kwa sasa anatarajiwa kuwa mchezaji huru mwishoni mwa mwezi huu, pamoja na winga Leandro Trossard.
Arsenal walimpa Partey kile walichokiona kuwa ni ofa ya ushindani takriban siku 10 zilizopita lakini kwa sasa bado hakuna makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande hizo mbili.
Kiungo huyo kutoka Ghana, ambaye atatimiza miaka 32 Ijumaa ijayo anataka kuendelea kusalia na Arsenal licha ya kupokea ofa za timu kadhaa kutoka Hispania ikiwemo Barcelona.
Hata hivyo, inasemekana Partey anasitasita kwa kuwa mkataba wake ujao huenda ukawa ndiyo wa mwisho mkubwa maishani mwake, hivyo anataka mpunga wa maana.
Pande zote zinataka kupata suluhisho la haraka kwani Partey na wakala wake Jose Daniel Jimenez Pozanco, ambaye ndiye anayeshughulikia mazungumzo na Arsenal, wanatarajiwa kuwa Ghana kati ya Juni 10 hadi Juni 13 kwa ajili ya shindano la pili la ‘Thomas Partey tournament’ ambapo maskauti kutoka Ulaya watafanya tathmini ya vipaji vya vijana.
Vile vile, Partey anatarajiwa kushiriki katika tamasha la All Star Festival huko Accra, Ghana Juni 18.