Argentina yaepuka adhabu kali ya FIFA, Paredes afungiwa mechi 10
Muktasari:
- Hata hivyo, Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) limemfungia kiungo wa Argentina, Leandro Paredes, mechi 10 kutokana na ugomvi uliozuka mwishoni mwa fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Hispania, huku mwenzake Nahuel Molina akifungiwa mechi saba.
ZURICH, USWISS; ARGENTINA imeepuka adhabu kubwa licha ya shinikizo la kuitaka iwaadhibu nyota wake waliobeba bango lililodai kuwa Visiwa vya Falkland ni sehemu ya nchi hiyo, baada ya ushindi wao wa nusu fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya England mwezi uliopita.
Hata hivyo, Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) limemfungia kiungo wa Argentina, Leandro Paredes, mechi 10 kutokana na ugomvi uliozuka mwishoni mwa fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Hispania, huku mwenzake Nahuel Molina akifungiwa mechi saba.
Hata hivyo, Argentina, ambayo ilimaliza ikiwa mshindi wa pili wa mashindano hayo, imeepuka adhabu kali ilipofika suala la maandamano yao kuhusu Visiwa vya Falkland.
FIFA imeiwekea Argentina adhabu ya kufunga sehemu ya uwanja kwa mechi mbili, hatua itakayopunguza idadi ya mashabiki watakaoruhusiwa kuhudhuria mechi mbili zijazo za nyumbani hadi asilimia 50 ya uwezo wa uwanja. Hata hivyo, moja ya adhabu hizo imesitishwa.
Pia Argentina imepigwa faini ya pauni 235,000, ambapo pauni 73,000 kati ya hizo zimesitishwa.
Bango hilo, ambalo lilionyeshwa kwa mara ya kwanza na mashabiki kabla ya kushushwa na kukabidhiwa wachezaji baada ya kuifunga England kwa mabao 2-1, lilikuwa limeandikwa kwa lugha ya Kihispania: “The Falkland Islands are Argentine”, likimaanisha “Visiwa vya Falkland ni vya Argentina.”
Licha ya FIFA kuwa na sheria zinazopiga marufuku bendera na alama za kisiasa, nahodha wa zamani wa Tottenham, Cristian Romero, beki wa Manchester United, Lisandro Martinez, pamoja na kiungo wa zamani wa Spurs, Giovani Lo Celso, walionekana kusherehekea wakiwa na bango hilo baada ya filimbi ya mwisho.
Nahodha na nyota wa Argentina, Lionel Messi, naye alionekana akicheza sambamba na bango hilo.
Waziri wa Masuala ya Biashara wa Uingereza, Peter Kyle, alisema kitendo cha kupeperusha bango hilo kilikuwa “hakifai kabisa”, huku akiisifu England kwa kuonyesha heshima na nidhamu, akisema ilikuwa tofauti kubwa na kile kilichoonekana kutoka kwa kikosi cha Argentina.
Paredes alimshika shingoni mchezaji wa Hispania, Eric Garcia, kabla ya kumpiga Gavi usoni na kumsukuma chini katika tukio lililoacha taswira mbaya baada ya mchezo kumalizika.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 sasa atakosa mechi 10 zijazo za Argentina, huku pia akitozwa faini ya pauni 65,000.
Molina naye alihusika katika vurugu hizo baada ya kumpiga nahodha wa Hispania, Rodri, sehemu ya tumboni alipokuwa akikimbia. Kitendo hicho kilimfanya kiungo huyo kugeuka na kumkabili mpinzani wake.
FIFA imemfungia Molina mechi saba kutokana na tukio hilo.
Wakati huohuo, Thiago Almada wa Argentina na Gavi wa Hispania watatumikia adhabu ya kufungiwa mechi moja kila mmoja kutokana na ushiriki wao katika matukio hayo yaliyokiuka misingi ya uanamichezo.
Hata hivyo, faini hizo hazitakuwa na athari kubwa kwenye fedha ambazo Argentina ilipata baada ya kumaliza katika nafasi ya pili nchini Marekani Kaskazini, kwani iliondoka na zawadi ya pauni 25 milioni.