Angola yatinga fainali Futsal Afcon 2026
Muktasari:
- Ushindi huo wa nusu fainali uliopatikana juzi katika Uwanja wa Moulay Abdellah Sports Hall, Rabat, umeiwezesha Angola kutinga fainali itakayochezwa leo Jumatano, Oktoba 21, 2026.
RABAT, MOROCCO: ANGOLA imeonyesha uwezo mkubwa wa kupambana baada ya kutoka nyuma kwa mabao 2-0 na kuichapa Algeria 3-2, na hivyo kufuzu fainali ya michuano ya TotalEnergies CAF Futsal AFCON Morocco 2026.
Ushindi huo wa nusu fainali uliopatikana juzi katika Uwanja wa Moulay Abdellah Sports Hall, Rabat, umeiwezesha Angola kutinga fainali itakayochezwa leo Jumatano, Oktoba 21, 2026.
Algeria, iliyokuwa ikishiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza katika historia yake, ilionekana kuwa na nafasi kubwa ya kusonga mbele baada ya kutawala kipindi cha kwanza na kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Mathieu Hammad aliifungia Algeria bao la kwanza dakika ya tisa kupitia mpira wa adhabu, kabla ya Ait Hamadouche kuongeza la pili dakika ya 19 na kuifanya Angola kuwa katika wakati mgumu.
Hata hivyo, Angola ilirejea kipindi cha pili ikiwa na nguvu mpya na kuanza kulisakama lango la wapinzani wake.
Aderito Santos aliipa Angola matumaini baada ya kupunguza pengo dakika ya 29, kabla ya Hornes Do Santo kusawazisha dakika ya 35 na kuufanya mchezo kuwa sare ya mabao 2-2.
Wakati mchezo ukionekana kuelekea dakika za nyongeza, Francisco Gabriel Chico aliibuka shujaa wa Angola kwa kufunga bao la tatu dakika ya 38, akiwapa timu yake uongozi wa kwanza na hatimaye ushindi wa mabao 3-2.
Hali ya Algeria ilizidi kuwa ngumu baada ya Amar Bessa kuonyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa mchezo kwa kumchezea rafu ya hatari Joao Cambangula.
Filimbi ya mwisho ilithibitisha ushindi muhimu kwa Angola, ambayo sasa imebakiza hatua moja kutwaa ubingwa wa Afrika wa futsal.
Angola itashuka dimbani leo Jumatano, usiku kucheza fainali dhidi ya Morocco, ambayo iliichapa Misri mabao 6-0.
Kwa upande wa Algeria, itashiriki mchezo wa kutafuta mshindi wa nafasi ya tatu utakaochezwa siku hiyo hiyo kuanzia saa 5:00 usiku dhidi ya Misri.