Chombo: Ndoto za jeshi zilizimwa na ajali
Muktasari:
- Mwanaspoti limefanya mahojiano na Chombo ambaye ni mchezaji wa klabu ya Sauti Parasport na timu ya taifa ya Tanzania soka la walemavu anasimulia tukio lililomtokea hadi likapelekea kukatwa mguu mmoja.
MWANASOKA mwenye ulemavu wa mguu mmoja Salim Chombo simulizi yake inaweza kukutoa machozi na kufunza jambo, hakutarajia ingetokea siku atapoteza moja ya kiungo chake lakini ghafla alijikuta katika hali ya sintofahamu iliyokatiza ndoto zake za kuwa mwanajeshi.
Mwanaspoti limefanya mahojiano na Chombo ambaye ni mchezaji wa klabu ya Sauti Parasport na timu ya taifa ya Tanzania soka la walemavu anasimulia tukio lililomtokea hadi likapelekea kukatwa mguu mmoja.
"Binadamu ukiwa mzima huo ni utajiri tosha hata kama tunakuwa na uhitaji wa baadhi ya vitu katika maisha yetu lakini wakati wa kukosa lazima umshukuru Mungu kwa kila jambo maisha yana sapraizi nyingi ambazo huwezi kuzitarajia hilo ndilo lililotokea kwangu na lilinifunza siri za Mwenyezi Mungu zinatisha," anasema.
MWAKA 2006 ULIMUACHIA MAJONZI
Chombo anasema mwaka 2006 hatausahau katika maisha yake ambapo baada ya kupata ajali alikatwa mguu:"Nakumbuka siku hiyo niliamka kwa shangwe na kuongozana na kaka yangu kwenda shambani kaka alikuwa amebeba manati ya kupigia ndege kwa watu walioishi mikoani wanajua kwamba unakamata ndege kisha ukirudi nyumbani unamchoma na kula.
Anasema: "Wakati tunarejea nyumbani kaka alikuwa anapiga ndege mimi nilikuwa naokota mawe ya kuweka kwenye manati kwa ajili ya kupigia ndege kaka alikuwa ameishavuka barabara anamkimbiza ndege aliniacha nyuma naokota mawe wakati navuka barabara nikateleza na kujikuta gari limenipitia mguuni yalikuwa yale ya ujenzi wa barabara nilizimia baada ya kushituka nikajikuta nipo kwenye taski nikazimia tena kuamka mara ya pili nikajikuta nipo Dar es Salaam hospitali.
"Nakumbuka nilikuwa nazungumza Kizigua baada ya kuamka nikawa nadai mguu wangu maana nilikuwa siuoni sasa nikawa na vurugu za kuchanganyikiwa baada ya kukaa kwa muda hospitali na kupona nikaruhusiwa kwenda nyumbani nilikuwa natembelea magongo.
"Nilikuja kuizoea hali ya ulemavu baada ya kupelekwa kusoma shule ya msingi ya Kikristo la Jeshi la Wokovu iliyopo Dar es Salaam nilianza 2007 nikamaliza nikamaliza 2013 hiyo ni ya walemavu tu wengine ni walemavu zaidi yangu hilo likanifanya nione hali yangu ni ya kawaida.
"Akili ikawa inajijenga kwamba sipo peke yangu wanafunzi wenzangu walikuwa na furaha halafu ni shule ambayo ilikuwa inasimamia zaidi michezo nilikuwa napenda sana soka kabla sijaumia basi nilipoona jeshi halitawezekana nikaamua kujikita na mpira wa miguu."
Anasema kuhusu elimu pia safari yake haikuwa rahisi
"Baada ya kumaliza darasa la saba mwaka 2013 sikufanikiwa kuingia kidato cha kwanza 2014 baada ya kukosekana kwa ada hadi 2015 ndipo nikaanza kusoma kidato cha kwanza nikamaliza 2018 hivyo sikubahatika kuendelea tena," anasema.
"Soka limenipa heshima nimefika sehemu ambazo sikutarajia kuzifika nilianza kuichezea timu ya taifa 2019 ambapo tulisafiri kwenda kucheza michuano Angola kwenye michuano ya Afrika mwaka 2022 pia niliitwa timu ya taifa ambapo ilikuwa inashiriki michuano ya Kombe la Dunia nchini Uturuki baada ya hapo kuna klabu ya nchi hiyo ilivutiwa na kipaji changu ikawa imenisajili nikachezea kuanzia 2022 hadi 2023 nikarejea nyumbani."
MAGONGO YA KUCHEZEA, AOMBA MSAADA
Mchezaji huyo anasema anapenda kusaidiwa vifaa vya kuchezea mchezo huo kwa watu wenye ulemavu.
"Magongo ya kuchezea ambayo kwetu ni moja ya kifaa muhimu yanaanzia Shilingi 40 000 hadi 60,00 yanauzwa bei kwa uchumi wetu ambao tunajikongaja," anasema.
Mbali na hilo anazungumzia michuano ya Azam TV Amputee Football Tournament 2025 kwamba alicheza mechi zote akiwa na majeraha nyuma ya goti na alifanikiwa kumaliza akiwa na mabao saba na kinara alikuwa na 11 lakini bado anaendelea kusikilizia maumivu baada ya kukosa pesa ya matibabu.
"Changamoto ninayoipitia kwa sasa ni maumivu ya majeraha sinahitajika pesa ndefu ambazo sina kama kuna Watanzania ambao watanisapoti basi watakuwa wamenisaidia ili nipone niendelee na kazi ambayo inanisaidia kuendesha maisha yangu" anasema Chombo na kuongeza;
"Haijalishi nina mguu mmoja, mwanaume lazima upambane maana nyuma yako unakuwa unategemewa na watu wengi, lakini pia lazima nijijenge kwa ajili ya maisha yangu ya baadaye, maana lazima nitakuja kuwa na familia iliyo chini yangu siyo ya wazazi kwa maana ya baba na mama."
MAHUSIANO KUISHIA NJIANI
Akizungumzia suala la mahusiano, Chombo anasema amewahi kuwa na wasichana wawili kwa nyakati tofauti, lakini maisha hayakuwa kama alivyotarajia.
"Kuhusu mahusiano wasichana wawili niliachana nao kila mmoja kwa wakati wake kwa sababu ya kukosa pesa za kuwatunza, walishindwa kuvumilia," anasema.
"Lakini, kuhusu hali yangu kwao haikuwa shida ujue mwakamke siyo mtu wa kuvumilia shida kama ilivyo kwa wanaume," anasema Chombo anayemkubali Clatous Chama wa Simba na Clement Mzize wa Yanga.