Anayesakwa na Arsenal apiga bonge la bao
TURIN, ITALIA. STAA anayesakwa na Arsenal, Kenan Yildiz amefunga bao matata kabisa la juhudi binafsi wakati alipoisaidia Juventus kuichapa Frosinone 2-1 kwenye Serie A wikiendi iliyopita.
Kinda huyo wa kimataifa wa Uturuki mwenye umri wa miaka 18, hilo lilikuwa bao lake la kwanza kuifungia Juventus, huku akifanya hivyo katika staili ya kipekee kabisa.
Yildiz alichukua mpira kutoka upande wa kushoto nje ya penalti boksi, akakokota kuwapita mabeki watatu wa Frosinone, kabla ya kupiga shuti la chinichini kumpita kipa Stefano Turati.
Yildiz anafanya mambo hayo wakati huu Arsenal ikihitaji saini yake ili akakipige kwenye kikosi hicho cha Emirates. Kocha, Mikel Arteta anataka kuboresha kikosi chake kwenye dirisha la Januari ili kuhakikisha timu yake inaendelea kupambana na kuwa kwenye nafasi za juu kwenye msimamo hadi mwisho.
Mkataba wa sasa wa Yildiz utafika tamati Juni 2027, hivyo Arsenal italazimika kuweka mezani mkwanja wa maana kuwashawishi Juventus kumuuza mchezaji wao.
Kocha wa Juventus, Massimiliano Allegri amemsifia kinda huyo na kusema: "Kwa maoni yangu, atakuwa mchezaji mzuri sana."
Yildiz, ambaye aliachana na Bayern Munich mwaka jana, aliitwa kuichezea timu ya wakubwa ya Uturuki, Oktoba mwaka huu na Novemba alifunga bao lake la kwanza kwenye soka la kimataifa wakati Uturuki ilipoichapa Ujerumani mabao 3-2.
Arsenal inasaka pia saini za wachezaji Ivan Toney, Pedro Neto na Douglas Luiz na wakali wote hao itajaribu kuwasajili kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya baridi huko Ulaya.