Amorim hana presha, yuko freshi tu!
Muktasari:
- Kwa kipindi hicho Man United haikuwa na mechi yoyote. Na ndio maana hakukuwa na habari za bilionea Sir Jim Ratcliffe na familia ya Glazer, wamiliki wa klabu ya Man United juu ya kumpiga chini kocha Ruben Amorim, ambaye ameshinda mechi 20 tu kati ya 50 za kwanza alizoinoa timu hiyo yenye maskani yake Old Trafford.
LONDON, ENGLAND: WAKATI wa mapumziko ya mechi za kimataifa, umesikia mengi kuhusu Manchester United.
Kulikuwa na uvumi kuhusu klabu hiyo kuwapo kwenye uwezekano wa kuuzwa, habari za kuhusu ujenzi wa uwanja mpya utakaoingiza mashabiki 100,000 na kuhusu kupanda kwa hisa za Man United katika soko la hisa New York na kuifanya miamba hiyo ya Old Trafford kupiga pesa ndefu.
Kwa kipindi hicho Man United haikuwa na mechi yoyote. Na ndio maana hakukuwa na habari za bilionea Sir Jim Ratcliffe na familia ya Glazer, wamiliki wa klabu ya Man United juu ya kumpiga chini kocha Ruben Amorim, ambaye ameshinda mechi 20 tu kati ya 50 za kwanza alizoinoa timu hiyo yenye maskani yake Old Trafford.
Kwa kipindi hiki mabosi wa Man United wanaonekana kuwa bize kwenye harakati za ujenzi wa uwanja, kupanua wigo wa mapato kupitia dili za kibiashara na taarifa za kudaiwa timu kupata mnunuzi.
Kutokana na hayo, Amorim sasa atakuwa na muda wa kutosha wa kufanya mambo yake bila kuwa na hofu ya kufunguliwa mlango wa kutokea huko Old Trafford. Mabilionea wamiliki wa klabu hiyo, familia ya Glazer na Ratcliffe wanafurahishwa na mambo yanayoendelea nje ya uwanja kwa sababu klabu inapiga pesa na kupata dili kubwa za kibiashara na ndiyo maana tajiri Ratcliffe kuibuka na kudai Amorim anastahi kupewa muda mrefu, pengine zaidi ya miaka mitatu ili kuonyesha ubora wake.
Na hilo lina maana Amorim ataendelea kuwa salama hata kama kikosi chake kitakumbana na kipigo kizito kutoka kwa Liverpool huko Anfield.
Kwa upande wa mashabiki ni kitu kigumu kumvumilia Amorim endapo kama atakumbana na kipigo kizito huko Anfield, lakini kwa mabosi wake hali ni tofauti kabisa, maana kocha huyo alinusurika kupigwa kibuti baada ya kufungwa na Grimsby Town, hivyo haiwezi kuwa tatizo atakapopoteza mbele ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Liverpool.
Na ikizingatiwa kwamba Liverpool ya Arne Slot imetoka kupoteza mechi tatu mfululizo, hivyo itahitaji ushindi wa lazima kuliko hata Amorim anavyohitaji. Kinachoonekana kwa sasa Slot yupo kwenye presha kubwa ya kuhitaji matokeo ya ushindi katika mchezo huo kuliko Amorim.
Katika mchezo wa Jumapili huko Anfield, Amorim atakuwa kwenye nafasi kubwa ya kukiweka kibarua cha Slot kwenye matatizo makubwa kuliko wasiwasi wa kupoteza kazi yeye huko Old Trafford.
Bilionea Ratcliffe anaamini Amorim anahitaji muda wa kukijenga kikosi chake kama ambavyo mabosi wa Arsenal walifanya kwa Mikel Arteta na sasa miamba hiyo ya Emirates imekuwa kwenye orodha ya timu zinazoshindania ubingwa kwenye Ligi Kuu England na Ulaya.
Katika kuelekea mchezo ho, Slot amekuwa kwenye mtihani mzito katika kipindi hiki cha kuifanya Liverpool kucheza vizuri kufuatia kuvunja mara mbili rekodi ya uhamisho Uingereza kwenye usajili wa Florian Wirtz na Alexander Isak kwa zaidi ya Pauni 200 milioni.
Ni mechi ngumu kwa Slot, ambaye atakuwa kwenye presha kubwa ya kuhusu usalama wa kibarua chake kuliko Amorim.