Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Alonso akalia kutikavu Chelsea

ALONZO Pict

Muktasari:

  • Kipigo hicho kimeongeza wasiwasi kwa mashabiki wa Chelsea, ambao walionyesha hasira zao kwa kuizomea timu yao katika vipindi tofauti vya mchezo huo, uliokuwa ushindi wa kwanza wa Leeds ugenini dhidi ya Chelsea tangu mwaka 1999.

LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Chelsea, Xabi Alonso ameanza kukabiliwa na presha kubwa mapema katika jukumu lake, baada ya kikosi chake kukubali kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa Leeds United kwenye Uwanja wa Stamford Bridge.

Kipigo hicho kimeongeza wasiwasi kwa mashabiki wa Chelsea, ambao walionyesha hasira zao kwa kuizomea timu yao katika vipindi tofauti vya mchezo huo, uliokuwa ushindi wa kwanza wa Leeds ugenini dhidi ya Chelsea tangu mwaka 1999.

Zomeazomea za mashabiki zilianza kipindi cha mapumziko wakati matokeo yakiwa sare ya bao 1-1. Hali ilizidi kuwa mbaya baada ya Leeds kufunga mabao ya tatu na nne, huku baadhi ya mashabiki wakianza kuondoka uwanjani kabla ya mchezo kumalizika. Walioendelea kubaki walionyesha tena kutoridhishwa kwao baada ya filimbi ya mwisho.

Pamoja na Chelsea kuwa na sababu za kujitetea, ikiwamo uamuzi wa mwamuzi wa kutoa penalti ambao unaweza kuonekana kuwa mkali dhidi yao na kuumia kwa kiungo Moises Caicedo, aliyeungana na wachezaji wengine watano waliokuwa nje kwa majeraha, kipigo hicho kilistahili kutokana na kiwango kibovu walichoonyesha.

ALO 01

Matokeo hayo yanaifanya Chelsea kuwa imepoteza mechi tatu kati ya nne zilizopita za Ligi Kuu England, huku ikishuka kutoka nafasi ya tano hadi ya nane kwenye msimamo wa ligi, ikiwa tayari imeachwa kwa pointi 14 na vinara Arsenal.

Hiyo si mara ya kwanza kwa Chelsea kuonyesha udhaifu nyumbani msimu huu. Oktoba, Tottenham Hotspur iliibuka na ushindi Stamford Bridge kwa mara ya pili pekee katika zama za Ligi Kuu England, huku kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Sunderland, iliyokuwa mkiani mwa msimamo, kabla ya mapumziko ya mechi za kimataifa kikiwa ishara nyingine ya hatari.

Kwa mujibu wa takwimu za kihistoria, ni mara ya kwanza ndani ya miaka 67 kwa Chelsea kupoteza nyumbani dhidi ya Leeds na Tottenham katika msimu mmoja.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Alonso alikiri kuwa kikosi chake kinahitaji kutafuta suluhisho la changamoto zinazokikabili, hasa katika kukabiliana na presha wakati wa mchezo.

ALO 02

"Ni lazima tutafute suluhisho kwa sababu changamoto zinaweza kujitokeza wakati wowote katika mchezo. Ni muhimu kuweza kukabiliana nazo na kuelewa kuwa bado kuna muda mrefu wa kucheza.

"Hilo ni jambo la lazima katika mashindano haya, lakini leo nimehisi kuwa huenda kwa sasa timu yetu ipo katika kipindi cha udhaifu wa kisaikolojia.

"Tulipopigwa pigo, hatukuweza kurejea imara kama ilivyopaswa," amesema Alonso.

Ukweli ni kwamba hata katika michezo ambayo Chelsea imekuwa ikipata ushindi, haijaonyesha kiwango cha kuridhisha kwa uthabiti, hali inayozidi kuibua maswali kuhusu ubora na uimara wa kikosi hicho.

ALO 03

Hata hivyo, mashabiki wa Chelsea walikuwa na matumaini makubwa baada ya kuwasili kwa Alonso, ambaye jina lake lilikuwa likiimbwa na mashabiki wakati wa mwanzo wa safari yake klabuni hapo, licha ya timu hiyo kumaliza msimu uliopita katika nafasi ya 10.

Matumaini hayo yalichochewa pia na usajili wa wachezaji wapya katika dirisha la majira ya kiangazi, akiwamo Morgan Rogers, aliyesajiliwa kwa rekodi ya klabu ya Pauni milioni 117, pamoja na wachezaji wenye uzoefu Emiliano Martinez, Danny Welbeck na Jordan Henderson.

ALO 04

Hata hivyo, uwezo wa Rogers kufumania nyavu, sambamba na Cole Palmer na Joao Pedro mwanzoni mwa msimu, ulionekana kuficha udhaifu uliokuwapo ndani ya kikosi cha Alonso.

Kabla ya mechi za mwishoni mwa wiki, Chelsea ilikuwa nafasi ya 14 katika kipimo cha tofauti ya mabao yaliyotarajiwa kufungwa na kufungwa, huku ikiwa katika nafasi ya pamoja ya 12 kwenye jedwali la pointi zilizotarajiwa kwa mujibu wa takwimu za Opta.

Akizungumzia kiwango cha Chelsea baada ya kipigo hicho, mshambuliaji wa zamani wa England na mchambuzi wa kipindi cha Match of the Day cha BBC, Alan Shearer, amesema timu hiyo ilionekana kupoteza mwelekeo kabisa.

ALO 05

"Chelsea ilikuwa imechanganyikiwa kila upande. Baada ya Moises Caicedo kuumia mapema na kutoka uwanjani, timu ilikosa nguvu za kimwili na ilionekana dhaifu.

"Hawakutengeneza nafasi nyingi za kufunga, huku safu yao ya ulinzi ya wachezaji wanne ikionekana kutokuwa na utulivu. Hakukuwa na ari, mshikamano wala mapambano kutoka kwa wenyeji, lakini hilo lisipunguze sifa za Leeds kwa ushindi wao.

"Wiki mbili zilizopita Chelsea ilizidiwa nguvu na mshambuliaji wa Sunderland, Brian Brobbey, na leo imeruhusu Dominic Calvert-Lewin kufanya jambo hilo hilo. Hilo linatia wasiwasi.

"Ni wazi kuwa kipindi cha mwanzo cha mafanikio na matumaini ya Alonso kimeisha. Anapaswa kuwaambia wachezaji wake kuwa kiwango hiki hakikubaliki. Wapo mbali sana na kiwango kinachohitajika na wanapaswa kuboresha kila eneo la mchezo," amesema Shearer.