Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

EPL leo kama jana

Muktasari:

  • Kwa hiyo, hebu linganisha jinsi timu zinavyofanya vizuri msimu huu na zilivyokuwa katika hatua kama hiyo msimu uliopita wa 2025/26. Ni mambo gani makubwa yaliyojitokeza? Hebu angalia kwa karibu.

ZIMESHACHEZWA mechi 10 katika Ligi Kuu England msimu wa 2026/27, na sasa ni mapumziko ya pili na ya mwisho ya kimataifa kwa mwaka huu. Inaonekana mechi 10 ni idadi nzuri ya kuanza kutathmini mwenendo wa timu.

Kwa hiyo, hebu linganisha jinsi timu zinavyofanya vizuri msimu huu na zilivyokuwa katika hatua kama hiyo msimu uliopita wa 2025/26. Ni mambo gani makubwa yaliyojitokeza? Hebu angalia kwa karibu.


ARSENAL PALE JUU

Arsenal inaongoza msimamo kama ilivyokuwa baada ya mechi 10 msimu uliopita. Hata hivyo, imekuwa na kiwango bora zaidi msimu huu, ikipoteza pointi katika mchezo mmoja tu, iliposhangaza kwa kufungwa na Brighton mabao 3-0.

Pointi 27 ilizonazo ni mbili zaidi ya ilizokuwa nazo katika hatua kama hii msimu uliopita. Hilo linaashiria matumaini makubwa kwa kikosi hicho, ikizingatiwa kwamba kilimaliza kwa kutwaa ubingwa. Ni timu nne pekee katika historia ya Ligi Kuu England zilizokusanya pointi nyingi zaidi katika mechi 10 za kwanza za msimu; Chelsea 2005/06, Manchester City 2011/12, Manchester City 2017/18 na Liverpool 2019/20. Zote zilikuwa na pointi 28 na zote zilimaliza kwa kutwaa ubingwa.


MAAJABU YA BRIGHTON

Brighton imekuwa timu iliyoshangaza zaidi msimu huu, ikikusanya pointi 22 katika mechi 10 za kwanza. Jumla hiyo ni pointi saba zaidi ya ilizokuwa nazo baada ya mechi 10 msimu wa 2025/26, ikiwa ndiyo tofauti kubwa zaidi ya ongezeko la pointi kwa timu yoyote katika ligi.

Pia, imepanda nafasi nane ikilinganishwa na ilipokuwa baada ya mechi 10 msimu uliopita iliposhika nafasi ya 10. Hilo ni ongezeko kubwa zaidi la nafasi kwa pamoja na Everton, ambayo imepanda kutoka ile ya 14 katika hatua kama hiyo msimu uliopita hadi sita kwa sasa.

Pointi 22 za Brighton ni nyingi zaidi kuwahi kukusanya katika mechi 10 za kwanza za kampeni yoyote ya ligi ya daraja la juu. Ni katika msimu wa 1953/54 wa Third Division South pekee ambapo ilikuwa na pointi nyingi zaidi katika hatua hii ya msimu wa ligi, baada ya kuhesabu ushindi kuwa pointi tatu. Wakati huo ilikuwa na pointi 23.


MDOGOMDOGO

Ni timu saba pekee kati ya 17 zilizoshiriki misimu yote miwili ya Ligi Kuu England ambazo zina pointi nyingi zaidi msimu huu kuliko zilivyokuwa nazo katika hatua kama hiyo msimu uliopita. Hilo linaonyesha jinsi ilivyo vigumu kudumisha kiwango cha matokeo katika ligi ya daraja la juu England. Kama ilivyotajwa, Everton ni mojawapo ya timu hizo.

Kikosi hicho cha David Moyes kiko nafasi nane juu na kina pointi nne zaidi ya kilivyokuwa katika hatua kama hii msimu uliopita. Mara ya mwisho Everton ilipokusanya pointi nyingi zaidi katika mechi 10 za kwanza za msimu ilikuwa 2016/17 ilipokuwa nazo 17 na mwishoni mwa msimu ilimaliza nafasi ya saba.

Leeds ina pointi tatu zaidi ya ilivyokuwa katika hatua kama hiyo msimu uliopita, jambo linaloonyesha kuboreka kwa kiwango chake msimu huu.

Labda jambo la kushangaza zaidi ni kwamba, Nottingham Forest nayo ina pointi tatu zaidi ya ilizokuwa nazo katika hatua hii msimu uliopita, licha ya kuanza kampeni hii kwa kiwango ambacho hakijafurahisha kwa kiasi kikubwa. Ilikuwa na pointi tisa dhidi ya sita.

Forest ilionyesha kiwango bora katika ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Manchester City, wikiendi iliyopta, na huenda hatimaye inaanza kuona bahati ikibadilika baada ya kutumia sehemu kubwa ya msimu ikiwa upande usiofaa wa takwimu za mabao yanayotarajiwa.

Ukizungumzia Manchester City, imepoteza mechi zake tatu za mwisho mfululizo, lakini kocha Enzo Maresca ana pointi mbili zaidi kuliko Pep Guardiola alizokuwa nazo katika hatua kama hii msimu uliopita. Maresca ana pointi 21 dhidi ya 19 za Guardiola.

Brentford ina pointi moja zaidi msimu huu, huku Liverpool (18) na Newcastle (12) zikiwa na jumla zinazolingana na zile za msimu uliopita.

HALI MBAYA

Kwa upande wa timu zinazofanya vibaya zaidi, zipo tatu. Sunderland ilipata ushindi mkubwa wa 1-0 dhidi ya Chelsea kabla ya kalenda ya mapumziko ya Fifa ulioiondoa katika nafasi za chini za msimamo. Hata hivyo, bado haifanyi vizuri ikilinganishwa na ilipokuwa katika hatua kama hii msimu uliopita. Ina pointi 10 chache, ikiwa na pointi nane dhidi ya 18, na iko nafasi 15 chini katika msimamo ikiwa ya 19 ikilinganishwa na nafasi ya nne msimu uliopita. Hiyo ndiyo rekodi mbaya zaidi kwa timu zote katika vipengele hivyo viwili.

Pierre Sage ameshapoteza kazi yake Crystal Palace. The Eagles iko mkiani mwa msimamo ikiwa na pointi saba pekee baada ya mechi 10. Hizo ni pointi tisa pungufu ya zile za mtangulizi wake, Oliver Glasner, alizokuwa amepata katika hatua kama hiyo ya msimu wa 2025/26.

Kwa namna Manchester United inakabiliwa na mwanzo mbaya zaidi kuwahi kuwa nao katika Ligi Kuu England, kwa hiyo haishangazi jumla ya pointi zake imeshuka ikilinganishwa na msimu uliopita. Hata hivyo, tofauti hiyo ni kubwa, ikiwa pointi nane dhidi ya 17, pungufu ya pointi tisa ilizokuwa nazo 2025/26.

ZINGINE HIZI HAPA

Tottenham Hotspur inaweza kuwa imeshinda mechi tatu kati ya nne zilizopita, lakini ushindi wake wa kwanza katika mfululizo huo haukuja hadi mchezo wake wa saba wa msimu. Ilikuwa imetoka sare tatu na kupoteza mechi tatu katika michezo yake sita ya mwanzo.

Mwanzo huo wa taratibu unamaanisha Spurs bado ina pointi tano pungufu ya ilizokuwa nazo baada ya mechi 10 msimu uliopita, ambapo iliendelea hadi kuepuka kushuka daraja katika siku ya mwisho ya msimu.

LONDON, England: Bournemouth iko katika kiwango cha kuvutia, ikiwa imeshinda mechi nne mfululizo za Ligi Kuu England na hivyo kulingana na rekodi yake ndefu zaidi ya ushindi mfululizo katika mashindano hayo. Hata hivyo, mwanzo wake wa taratibu katika mechi sita za kwanza unamaanisha bado ina pointi tatu pungufu ya zile 18 ilizokuwa nazo katika hatua kama hii msimu uliopita.

Aston Villa kwa upande wake ina pointi mbili pungufu, Fulham pointi moja pungufu na Chelsea nayo pointi moja pungufu ikilinganishwa na zilivyokuwa baada ya mechi 10 msimu wa 2025/26.