Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ajali ya treni yaahirisha mechi 24 Hispania

SPAIN Pict

Muktasari:

  • Ajali hiyo imesababisha majonzi nchini Hispania, huku klabu kubwa za soka zikiwemo Real Madrid, Barcelona na Atlético Madrid zikitoa salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na kuwatakia nafuu ya haraka majeruhi.

MADRID, HISPANIA: SHIRIKISHO la Soka la Hispania (RFEF), limeahirisha mechi zote 24 za Copa del Rey zilizopangwa kuchezwa leo Jumatano, kufuatia ajali ya treni mbili iliyotokea saa 2:54 asubuhi kwa saa za Hispania katika eneo la Toledo lililopo katikati mwa nchi hiyo, iliyosababisha vifo vya watu wasiopungua 30 na wengine takribani 80 kujeruhiwa.

Ajali hiyo imesababisha majonzi nchini Hispania, huku klabu kubwa za soka zikiwemo Real Madrid, Barcelona na Atlético Madrid zikitoa salamu za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao na kuwatakia nafuu ya haraka majeruhi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na shirika la habari la Associated Press (AP), ajali hiyo ilitokea baada ya treni ya mwendo kasi kugonga sehemu ya nyuma ya treni nyingine iliyokuwa imesimama kwenye reli. Mamlaka zilisema idadi ya waliofariki inaweza kuongezeka kutokana na ukubwa wa ajali hiyo.

SPA 01
SPA 01

Kupitia taarifa yake, RFEF ilieleza kuwa uamuzi wa kuahirisha michezo hiyo umefikiwa kwa lengo la kuonesha mshikamano na waathirika wa janga hilo.

“Tumeshtushwa na ajali hii ya kutisha ya treni,” imesema taarifa ya shirikisho hilo.

RFEF iliongeza kuwa, imeamuru kuahirishwa kwa mechi hizo ili kutoa mshikamano na waathirika, huku ikieleza kuwa jumuiya nzima ya soka nchini Hispania imeungana katika majonzi na iko tayari kushirikiana na mamlaka kuwasaidia walioathirika.

Shirikisho hilo lilisema ratiba mpya ya michezo iliyoahirishwa itatangazwa baadaye, huku mechi zilizopangwa Alhamisi zikiendelea kusubiriwa kwa mujibu wa ratiba ya awali, kwani hazikuwa zimeahirishwa wakati wa kutolewa kwa taarifa hiyo.

SPA 02

Miongoni mwa michezo iliyokuwa imepangwa kuchezwa Jumatano ni Navalcarnero dhidi ya Real Betis, Salamanca dhidi ya Celta Vigo na Tavernes dhidi ya Valencia.

Kufuatia ajali hiyo, Real Madrid imetoa taarifa rasmi ikieleza masikitiko yake makubwa na kutoa pole kwa familia na ndugu wa waliofariki, huku ikiwatakia nafuu majeruhi na kuonesha mshikamano kwa wote walioathirika pamoja na vikosi vya uokoaji.

Barcelona nayo imetumia akaunti yake rasmi ya mtandao wa kijamii wa X kutoa rambirambi kwa familia na marafiki wa waathirika, huku ikiomba majeruhi wapone haraka.

SPA 03

Kwa upande wake, Atlético Madrid imeeleza kuungana na familia zilizopoteza wapendwa wao na kuwatakia nafuu ya haraka wote waliojeruhiwa.

Wakati huohuo, huduma za dharura, zikiwemo zimamoto, ulinzi wa raia na wahudumu wa afya, zilitumwa eneo la ajali kuendeleza shughuli za uokoaji na kutoa huduma kwa majeruhi. Hospitali za karibu pia zilijiandaa kupokea waliojeruhiwa, huku mamlaka za eneo la Castilla-La Mancha zikianzisha mpango wa dharura wa kikanda.

Pamoja na kusitishwa kwa michezo hiyo ya Copa del Rey, Ligi Kuu ya Hispania haikuwa imetangaza kuahirishwa kwa mechi za mwishoni mwa wiki wakati wa taarifa hiyo.