Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Afrika mwendo wa kusuasua Kombe la Dunia

AFRIKA Pict

Muktasari:

  • Benin, inayoshiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza, ilikumbana na kipigo cha mabao 8-0 kutoka kwa Argentina katika Kundi A, huku Tanzania ikipigwa 5-1 na England katika Kundi B.

Wawakilishi wa Afrika wameanza kwa kusuasua katika Kombe la Dunia la Wanawake la U-20 linalofanyika nchini Poland, baada ya Benin na Tanzania kupata vipigo vya mabao mengi vilivyozua maswali kuhusu uwezo wa bara hilo kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.

Benin, inayoshiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza, ilikumbana na kipigo cha mabao 8-0 kutoka kwa Argentina katika Kundi A, huku Tanzania ikipigwa 5-1 na England katika Kundi B.

Matokeo hayo yanaonyesha changamoto ambayo timu za Afrika zinaendelea kukutana nayo zinapokabiliana na mataifa yenye historia na uzoefu mkubwa katika soka la wanawake.

Kipigo cha Tanzania kilikuwa cha kuumiza zaidi baada ya Princess Ademiluyi, mchezaji mwenye asili ya Nigeria anayeiwakilisha England, kuisaidia timu hiyo kuanza mchezo kwa kasi.

Ademiluyi aliifungia England bao la kwanza dakika ya tisa baada ya kupokea pasi kutoka kwa Lia Vivienne ambaye ana asili ya Tanzania.

England, ambayo ilishawahi kushinda medali ya shaba mwaka 2018 na inashiriki Kombe la Dunia la U-20 kwa mara ya tano, ilitawala sehemu kubwa ya mchezo huo.

AFRI 01

Mchezaji aliyeibuka kuwa nyota wa mchezo alikuwa Rachel Maltby, aliyefunga hat-trick, mabao yote matatu yakitokana na mikwaju ya penalti.

Maltby alifunga bao lake la kwanza dakika ya 15 baada ya Lidya Vivienne kuadhibiwa kwa kosa lililoifanya England kupewa penalti.

Dakika ya 43, Maltby alifunga tena kwa penalti baada ya Elizabeth Mutimi kuadhibiwa.

Mutimi alipewa adhabu nyingine dakika mbili baadaye, jambo lililompa Maltby nafasi ya kukamilisha hat-trick yake na kuongeza maumivu kwa Tanzania.

Tanzania ilifanikiwa kupata bao la kufutia machozi dakika ya 65 kupitia Jamila Mnuduka, lakini mchezaji huyo alilazimika kuondoka uwanjani dakika tatu baadaye baada ya kupata majeraha.


AFRI 02

TANZANIA SASA YAKUTANA NA CANADA

Kipigo hicho kimeifanya Tanzania kuwa katika hali ngumu kuelekea mchezo wake wa mwisho wa Kundi B dhidi ya Canada.

Kwa upande mwingine, England itakutana na Brazil katika mchezo unaotarajiwa kuwa kivutio kikubwa wa kundi hilo.

Brazil inaongoza Kundi B ikiwa na pointi sita baada ya kushinda mechi zake mbili, ikiwemo ushindi wa 3-0 dhidi ya Canada, wakati England ina pointi nne.

Kwa Tanzania, mchezo dhidi ya Canada utakuwa muhimu katika harakati zake za kujaribu kujiweka katika nafasi ya kufuzu hatua inayofuata.


AFRI 03

BENIN 8-0

Katika Kundi A, Benin ilipokea kichapo kizito baada ya kuchapwa mabao 8-0 na Argentina.

Kipigo hicho kimeiacha timu hiyo, inayoshiriki Kombe la Dunia la U-20 kwa mara ya kwanza, ikiwa na pointi moja tu kabla ya mchezo wake wa mwisho dhidi ya wenyeji Poland.

Poland inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi sita baada ya kuifunga Mexico 2-1.


AFRI 04

GHANA KWENYE PRESHA

Wawakilishi wengine wa Afrika, Black Princesses ya Ghana, nao wako kwenye presha katika Kundi C baada ya kupoteza 3-0 dhidi ya Ecuador katika mchezo wao wa kwanza.

Mchezo wa pili ilishinda kwa mabao 3-1 dhidi ya Jamhuri ya Korea hivyo mchezo wao wa mwisho dhidi ya Ufaransa inayoongoza kundi hilo na pointi nne utakuwa muhimu kwa timu hiyo inayotafuta historia ya kufuzu hatua ya 16 bora.

Ghana ambayo iko nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi ikikusanya pointi tatu itakutana na Ufaransa katika mchezo wake unaofuata huku ikiwa na kazi ya kufanya ili kurejesha matumaini ya kusonga mbele katika michuano hiyo.

Kwa wawakilishi kadhaa wa Afrika kuanza michuano kwa matokeo yasiyoridhisha, bara hilo sasa linahitaji mabadiliko makubwa katika michezo iliyosalia ya makundi ili kuepuka matokeo mengine ya kusikitisha katika michuano hiyo ya kimataifa ya vijana.

Michezo iliyosalia ya makundi sasa imebeba umuhimu mkubwa kwa matumaini ya Afrika kupata wawakilishi watakaofuzu hatua ya mtoano.