Sababu za kinywa kunuka, zingatia haya
Muktasari:
- Watu unaozungumza nao wanaweza kuanza kujisitiri kwa mikono, kugeuza nyuso zao au hata kutafuta sababu ya kuondoka, huku wewe ukibaki hujui kinachowafanya wasiwe huru kuwa karibu nawe.
Unaweza kuvaa nguo za bei ghali, kupaka marashi yenye harufu nzuri na kuhakikisha mwonekano wako umekaa nadhifu, lakini unapofungua kinywa na kutoa harufu mbaya, mambo yanaweza kubadilika ghafla.
Watu unaozungumza nao wanaweza kuanza kujisitiri kwa mikono, kugeuza nyuso zao au hata kutafuta sababu ya kuondoka, huku wewe ukibaki hujui kinachowafanya wasiwe huru kuwa karibu nawe.
Harufu mbaya ya kinywa ni tatizo linaloweza kumuathiri mtu yeyote, bila kujali umri au mwonekano wake.
Wakati mwingine hujitokeza asubuhi unapoamka, lakini kwa wengine huendelea hata baada ya kupiga mswaki. Tatizo hili linaweza kuathiri kujiamini, mawasiliano na mahusiano ya kijamii, hasa pale mhusika anaposhindwa kutambua chanzo chake.
Jambo la msingi ni kufahamu kuwa kupiga mswaki pekee hakutoshi kila wakati kuondoa harufu hiyo. Kuna sababu mbalimbali zinazoweza kuifanya mdomo unuke, kuanzia usafi usioridhisha wa kinywa hadi magonjwa ya meno, fizi na matatizo mengine ya kiafya.
- KUTOSAFISHA ULIMI NA MENO VIZURI
Hii ni miongoni mwa sababu kuu za harufu mbaya ya mdomo. Mabaki ya chakula yanapobaki katikati ya meno na juu ya ulimi, bakteria huyavunja na kutoa gesi zenye harufu isiyopendeza.
Ndiyo maana mtu anaweza kupiga mswaki lakini bado akawa na harufu mbaya ikiwa hasafishi ulimi na nafasi zilizo katikati ya meno.
Ili kupunguza tatizo hili, ni muhimu kupiga mswaki mara mbili kwa siku tena kwa utulivu mkubwa kwa dawa kusafisha ulimi na kutumia uzi maalumu wa kusafishia nafasi za meno.
- UKAVU WA MDOMO
Mate yana kazi ya kulainisha kinywa na kusaidia kuondoa mabaki ya chakula pamoja na bakteria. Mate yanapopungua, bakteria wanaohusishwa na harufu mbaya wanaweza kuongezeka.
Hali hii inaweza kutokea mtu anapokunywa maji kidogo, anapolala usiku au anapotumia baadhi ya dawa zinazopunguza uzalishaji wa mate.
- MAGONJWA YA MENO NA FIZI
Meno yaliyooza, fizi zinazovimba na maambukizi ndani ya kinywa yanaweza kusababisha harufu mbaya inayoendelea. Wakati mwingine, mabaki ya chakula na bakteria hujikusanya kwenye nafasi zilizoharibika na kuwa vigumu kuyaondoa kwa kupiga mswaki pekee.
Daktari wa meno anaweza kuchunguza chanzo na kupendekeza matibabu yanayofaa. Ikiwa fizi zinatoa damu mara kwa mara, kuna maumivu au uvimbe, ni muhimu kutafuta huduma ya kitaalamu badala ya kuficha harufu kwa kutumia marashi ya mdomo pekee.
- MATATIZO YA KOO NA PUA
Daktari Dorcas Natse mtaalamu wa kinywa anasema; “Maambukizi ya koo, mawe madogo yanayojikusanya kwenye tonsili na ute unaotiririka kutoka puani kuelekea kooni vinaweza kuchangia harufu mbaya ya mdomo.
Mawe ya tonsili, kwa mfano, yanaweza kuwa na harufu kali kutokana na mabaki ya chakula, bakteria na seli zilizokufa zinazojikusanya kwenye vijishimo vya tonsili.
Ikiwa harufu inaambatana na maumivu ya koo, matatizo ya kumeza au dalili nyingine zinazoendelea, ni vyema kumuona daktari kwa uchunguzi.”
5. TATIZO LA ASIDI YA TUMBO KUPANDA
Daktari Gilbert John anasema kuwa;”Kwa baadhi ya watu, asidi ya tumbo inapopanda kuelekea kwenye umio na koo, inaweza kusababisha ladha chachu au harufu isiyopendeza mdomoni. Hali hii hujulikana kama asidi ya tumbo kupanda kwenye umio.
Hata hivyo, si kila harufu mbaya ya mdomo husababishwa na tumbo. Mara nyingi chanzo huwa ndani ya kinywa, hivyo ni muhimu kuanza kwa uchunguzi wa meno na fizi kabla ya kuhitimisha kuwa tatizo linatokana na mfumo wa chakula.”