'Hata China, Pirates na Sundowns wana mashabiki'
Muktasari:
- Orlando Pirates na Mamelodi Sundowns, zote zikitokea Gauteng, zinatarajiwa kukutana katika fainali ya mwaka huu itakayopigwa Jumamosi, Oktoba 10, 2026.
DURBAN, AFRIKA KUSINI: KIPA wa zamani wa Orlando Pirates, Innocent Mayoyo, ameunga mkono uamuzi wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) kuandaa fainali ya Kombe la MTN8 kwenye Uwanja wa Moses Mabhida, Durban, akisisitiza kuwa uwanja huo ni wa upande wowote.
Orlando Pirates na Mamelodi Sundowns, zote zikitokea Gauteng, zinatarajiwa kukutana katika fainali ya mwaka huu itakayopigwa Jumamosi, Oktoba 10, 2026.
Hata hivyo, uamuzi wa kupeleka mchezo huo Durban umezua maswali kutoka kwa baadhi ya mashabiki, huku tiketi zote za fainali hiyo zikiwa tayari zimeuzwa.
Mchezo huo utakuwa fainali ya 11 ya Kombe la MTN8 kuandaliwa kwenye Uwanja wa Moses Mabhida tangu mwaka 2010.
Akizungumza na mtandao wa KickOff, Mayoyo alisema timu hizo zina mashabiki katika maeneo mengi duniani na kwamba kuchagua uwanja usioegemea upande wowote ni jambo linalofaa.
“Pirates na Sundowns zina mashabiki kila mahali, na Uwanja wa Moses Mabhida ni mahali sahihi kwa mchezo huu kwa sababu ni uwanja wa upande wowote,” alisema Mayoyo.
“Hata kama fainali hii ingefanyika China, uwanja ungejaa mashabiki wa Pirates na Sundowns. Klabu zote mbili zina mashabiki huko, hivyo kuandaa mchezo huu KwaZulu-Natal hakuwanyimi mashabiki wao fursa ya kuzitazama timu zao.
“Ikiwa lengo ni kuwahudumia watu, Uwanja wa Moses Mabhida ni mahali panapofaa kwa mchezo huu. Durban ina hoteli nyingi na sehemu mbalimbali za malazi, pamoja na shughuli za mapumziko. Tofauti na Johannesburg, Durban ni eneo maarufu la utalii, hivyo watu wanaweza kufanya mambo mengi zaidi.
“Mchezo unachukua dakika 90 pekee, kwa hiyo watu wengi wanaosafiri kwenda huko wanaweza kuwa na shughuli nyingine mbali na kutazama mpira. Cha muhimu ni kwamba mchezo unafanyika kwenye uwanja wa upande wowote.”