Kikosi Police pasua kichwa
USAJILI uliotisha ambao ulifanywa na Kenya Police FC bado haujaanza kulipa na hii ndiyo sababu ya kocha mkuu John Bobby Ogolla maarufu Six-Million-Dollar Man kung’aka baada ya mechi dhidi ya Wazito FC.
Kenya Police FC ambayo ilipanda Ligi Kuu Kenya msimu huu ilifanya usajili mkubwa mwanzoni mwa msimu na kisha kuimarisha tena kikosi chao katika dirisha dogo.
Hata hivyo matokeo uwanjani yamekuwa ya kususua na wikendi iliyopita walichezea kichapo cha mabao 3-2 kutoka kwa Wazito FC wakishika nafasi ya 13 na pointi 22.
Katika mechi sita za mwisho, Police FC wameshinda mechi moja, kupoteza miwili na kuambulia sare mechi tatu; kwa kifupi wamezoa pointi sita kati ya 18.
Mara ya mwisho vijana wa Ogolla kufurahia ushindi ilikua Januari 15 mwaka huu wakitoka nyuma na kushinda 2-1 dhidi ya Mathare United.
Safu ya ushambuliaji Police FC inaundwa na wachezaji nyota kama vile Clifton Miheso anayeongoza mbio za Kiatu cha Dhahabu na mabao 10, Elvis Rupia na Clinton Kinanga licha ya kumruhusu John Makwata kujinga na AFC Leopards kwa mkopo.
Aidha Police FC ‘ilivunja benki’ na kuwasajili wachezaji ambao wameshaitumikia Harambee Stars kama vile Haruna Shakava, Musa Mohammed, Duke Abuya, Francis Kahata na Duncan Otieno.
Lakini licha ya uwepo wa kikosi kilichosheheni wachezaji nyota matokeo ya mwishoni mwa wiki yalimkera kocha Ogolla akisema safu ya ushambuliaji inaona haya kutumia nafasi wanazotengeneza huku safu ya ulinzi ikiruhusu mabao kirahisi.
“Tumekuwa tukipoteza mechi kwa uzembe na makosa yanayoweza kuepukika. Timu imekuwa ikitengeneza nafasi lakini nakereka kuona hazitumike vyema. Pia tumekuwa tukiwapa zawadi ya mabao mepesi wapinzani wetu lakini tutaendelea kufanya kazi kama timu ili turudi kushinda mechi zetu,” alisema kocha Ogolla.
Moja wa wachezaji waliyomnyima raha Ogolla katika mechi dhidi ya Wazito FC ni kipa Ruben Juma hususan kwa mabao ya John Kuol na Amos Ekhalie na kulazimika kumtoa huku nafasi yake ikichukuliwa na Job Ochieng aliyejiunga na Police FC dirisha dogo la usajili akitokea Mathare United.
Hata hivyo, kocha Ogolla amesema ni vigumu kuondoa presha katika mchezo na kuwataka wachezaji wake kufanyia kazi maeneo dhaifu ili wamalize katika nafasi zinazoheshimika.
“Ushinde au upoteza, presha itakwepo tu. Nimezoea kufanya kazi zilizo na presha na nina imani tutarudi kuanza kushinda, wachezaji wanahitaji kujituma zaidi,” alisema mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa.