Huko mkiani mambo ni moto Kenya
MATHARE United na Vihiga Bullets zinachungulia kushushwa daraja Ligi Kuu Kenya huku ‘playoff’ ikiilenga Wazito FC wakati Nzoia Sugar bado hawapo salama.
Kwa mujibu wa kanuni za FKF-PL, timu mbili za mwisho zinashushwa daraja moja kwa moja na ile inayomaliza nafasi ya 16, yani ya tatu kutoka mwisho, inacheza mchezo wa mtoano na timu iliyomaliza nafasi ya tatu ligi daraja la kwanza maarufu National Super League nyumbani na ugenini.
Hadi FKF-PL inachukua mapumziko ya takribani wiki mbili, Mathare United inaburuza mkia ikiwa na pointi 11 wakizidiwa pointi nne na Vihiga Bullets huku Wazito FC iliyopo nafasi ya 16 imekijikusanyia pointi 20.
Timu nne ambazo zinapambana kuepuka rungu la kushuka daraja, zimebadilisha makocha wakiwa na matumaini ya kubadili matokeo yatakayowawezesha kuwa salama.
Kocha wa Vihiga Bullets, Juma Abdallah, anaamini mechi ambazo wamesalia nazo pindi mikikimikiki ya ligi itakaporudi sio ngumu isipokua safari ya kwenda Mombasa kuikabili Bandari FC.
“Ninaimani kubwa hivi karibuni tutaondoka eneo hili la timu zinazoshuka na tukijitahidi tutacheza ‘playoff’ lakini hayo ni kama tu mambo yataenda kama nilivyotazamia,” alisema Abdallah aliyekabidhiwa mikoba ya Vihiga Bullets iliyopanda daraja msimu huu baada ya kutimuliwa kwa Evans Mafuta.
Mwenye mawazo sawa Abdallah ni kocha wa Mathare United, John Kamau, ambaye amesisitiza huu sio muda wa mashabiki kuingiwa na taharuki akiwa na imani katika mechi 11 zilizobaki bado wanaweza kuepuka rungu la kushuka daraja.
Kamau aliyemridhi Ezekiel ‘Saachi’ Akwana amesema anaelewa kazi yake na hana hofu kama walivyo wengine huku akisisitiza ni mapema kuanza kuongea kuhusu kushuka daraja.
“Mechi tatu za mwisho tumeonyesha kandanda safi ukizingatia na namna timu ilivyokuwa inacheza nilipokabidhiwa, wachezaji wanaanza kuelewa nini tunachotaka kutoka kwao kiufundi,” alisema.
Naye kocha wa Wazito FC, Fred Ambani, amesema ni suala la muda tu timu yake kutinga nafasi ambazo zipo salama kwenye msimamo wa FKF-PL.
Ambani ambaye alikabidhiwa mikoba baada ya kutimuliwa kwa Francis Kimanzi amesema kila mtu kwenye klabu anafahamu hawapo kwenye nafasi nzuri na anaamini wanapambana kujinasua.
Tofauti na timu tatu zilizochini yao, Nzoia Sugar wapo kwenye mikono salama tangu Salim Babu kutua kumrithi Ibrahim Shikanda na timu hii kutoka Bungoma, hawajapoteza katika mechi zao nane za mwisho.
Kocha Babu yupo katika hali ya utulivu akiamini mafunzo aliyowapa vijana wake yanawafanya kuwa wakakamavu na kuwapa wakati mgumu wapinzani wao.