Zoran awatuliza mashabiki Simba

KOCHA wa Simba, Zoran Maki, amewatoa hofu wanachama, wapenzi na mashabiki wa klabu hiyo akiwaambia kwamba mechi yao ya leo ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga licha ya ugumu wake, lakini bado watatoboa kwa maandalizi mazuri iliyofanya tangu akabidhiwe timu.

Zoran atakayeiongoza Simba kwenye mechi ya kwanza ya mashindano tangu akabidhiwe timu akimpokea Pablo Franco, alisema Yanga ni timu nzuri kwa jinsi alivyokuwa akiifuatilia, lakini bado anaamini vijana wake wana nafasi kubwa ya kupindua meza kwa watani wao leo Kwa Mkapa.

Simba na Yanga zinavaana kwenye mechi hiyo itakayopigwa kuanzia saa 1:00 usiku ikichezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku zikiwa zimetoka kutesti mitambo kwenye mechi za kirafiki za kimataifa kupitia matamasha yao ya Wiki ya Mwananchi na Simba Day.

Msimu uliopita kwenye mechi kama hiyo, Simba ililala bao 1-0 lililowekwa kimiani na Fiston Mayele na Zoran alisema amedokezwa juu ya upinzani wa jadi wa timu hiyo, lakini kwake anaamini wachezaji wataenda kupambana ili kuanza msimu vizuri kabla ya kugeukia Ligi Kuu na ile ya CAF watakapokiwasha na Nyanza Bullets ya Malawi.

“Najua ni mechi ngumu, lakini kwa maandalizi tuliyoyafanya tangu tukiwa Misri na hata ya hapa Dar es Salaam na hasa mechi dhidi ya St George imetuongezea kujiamini na wachezaji wapo tayari kwa mchezo huo, hata kama ni mchezo huo ni mgumu na utakaokuwa na upinzani,” alisema Zoran na kuongeza;

“Hatuwadharau wapinzani wetu, kwani ni timu kubwa kama iluivyo Simba na ina wachezaji wazuri vilevile, lakini bado naiona nafasi ya Simba kupata matokeo mazuri na mashabiki na wapenzi wajitokeze kwa wingi kuisapoti timu yao kama walivyofanya Simba Day.”

Katika mechi ya Simba Day, Mnyama alishinda mabao 2-0 ya Kibu Denis na Nelson Okwa aliyekuwa akiitumikia kwa mara ya kwanza tangu ilipomsajili kutoka Rivers United.

Okwa na wachezaji wengine waliosajiliwa akiwamo Augustine Okrah, Victor Akpan, Nassor Kapama, Habib Kyombo, Mohamed Ouattara na Dejan Georgijevic kutoka Serbia wataliamsha sambamba na nyota waliosalia kwenye kikosi cha msimu uliopita.