Zimamoto yapunguzwa kasi Ligi Kuu Zanzibar
Muktasari:
- Zimamoto imepokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa bingwa mtetezi wa ligi hiyo, KVZ mechi iliyochezwa Uwanja wa Mao A uliopo Unguja.
HATIMAYE vinara wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), Zimamoto, imepoteza mchezo wake wa kwanza kwenye ligi hiyo baada ya kucheza mechi sita bila kupoteza.
Zimamoto imepokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa bingwa mtetezi wa ligi hiyo, KVZ mechi iliyochezwa Uwanja wa Mao A uliopo Unguja.
Katika mchezo huo, bao pekee la KVZ lilifungwa na mshambuliaji, Mudrik Abdi 'Gonda' dakika ya 77, akimalizia pasi ya mshambuliaji Mohammed Mussa 'Banega'.
Licha ya kufungwa mechi hiyo, bado Zimamoto imesalia nafasi ya kwanza katika msimamo ikiwa na pointi 16, inafuatia Uhamiaji na pointi 15 huku KVZ ikipanda hadi nafasi ya tatu ikikusanya pointi 13 ikiishusha Polisi iliyopo nafasi ya nne ikiwa na pointi 12.
Akizungumza baada ya kumalizika mchezo, Nahodha wa Zimamoto, Hussein Mwinyi amesema walitengeneza nafasi nyingi lakini walishindwa kuzitumia.
Alieleza kuwa, nafasi chache ambazo wapinzani wao walitengeneza walizitumia vyema hadi kufanikiwa kuwafunga.
"Tulitengeneza nafasi nyingi ambazo hatukuzitumia ipasavyo ikilinganishwa na KVZ walikuwanazo chache na kuzitumia inavyotakiwa," amesema.
Amesema, bado wana imani ya kuendelea kufanya vizuri, hivyo watarekebisha makosa uwanja wa mazoezi na kinachowapa nguvu zaidi ni kuongoza msimamo licha ya kufungwa.
Kwa upande wake, Nahodha na Kipa wa KVZ, Hamad Ubwa 'Baro' amesema wana kila sababu ya kutetea ubingwa wao kwani timu imeanza kurudi kwenye mfumo wake.
Amesema, hamasa ndio ilifanya kushinda mchezo huo baada ya kutoka kufungwa mechi iliyopita, wakajipanga vyema kuwadhibiti wapinzani wao.