Kiungo chipukizi ataka matokeo ZPL
Muktasari:
- Katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), Chipukizi ipo nafasi ya 15 chini ya Mwenge iliyopo nafasi ya 14 huku zote zikishinda mechi moja zikivuna pointi nne kwenye mechi sita ilizocheza.
KIUNGO mshambuliaji wa Chipukizi, Daddy Francis amesema sababu kubwa inayofanya timu hiyo kushindwa kupata matokeo mazuri ni mfumo ambao unacheza timu hiyo.
Amesema, kwa sasa Chipukizi inacheza mfumo wa kujilinda zaidi kuliko kushambulia hivyo huwafanya timu pinzani kuwashambulia wakati wote.
Ameeleza kuwa, katika mchezo dhidi ya Zimamoto uliochezwa Septemba 30, 2026, Chipukizi ilifungwa bao 1-0 kwa sababu ilifikia hatua baadhi wachezaji na kipa walichoka kuzuia mashambulizi.
“Timu inajilinda sana, kuliko kushambulia ndio maana tunafungwa, wachezaji wanachoka kuzuia mashambulizi ya timu pinzani hadi tunafungwa licha ya kupambana,” amesema
Amesema, timu ingekuwa inalinda na kushambulia hakuna sababu yakufungwa kwani tayari imeshakuwa nzuri na yenye muunganiko. Kiungo huyo, amesema timu haipo kwenye nafasi inayoridhisha na wachezaji wanapambana kupata matokeo mazuri lakini wanaambulia kufungwa na si kingine.
Amesema, anatamani kocha mkuu wa timu hiyo, Suleiman Mohamed ‘Mani Gamera’ kubadilisha mfumo kwa lengo la timu kupata matokeo kinyume na hapo mambo yatakuwa mabaya zaidi.
Chip ukizi itakaribishwa na Mwenge Oktoba 9,2026, kwenye Uwanja wa Gombani uliopo kisiwani Pemba huku zote zikichuana kutafuta ushindi.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), Chipukizi ipo nafasi ya 15 chini ya Mwenge iliyopo nafasi ya 14 huku zote zikishinda mechi moja zikivuna pointi nne kwenye mechi sita ilizocheza.