Singida BS yamvalia njuga Sowah
Muktasari:
- Hatua hiyo imekuja baada ya Sowah kutolewa nje dakika ya 88 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 kati ya Dodoma Jiji na Singida Black Stars, matokeo yaliyoifanya timu hiyo kufikisha pointi 11 baada ya mechi saba.
SINGIDA Black Stars imeamua kupitia tukio lililosababisha mshambuliaji wake, Jonathan Sowah, kuonyeshwa kadi nyekundu dhidi ya Dodoma Jiji FC huku Kamati ya nidhamu ya klabu hiyo ikitarajiwa kuamua hatua za kuchukua baada ya kutathmini mazingira ya tukio hilo.
Hatua hiyo imekuja baada ya Sowah kutolewa nje dakika ya 88 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliomalizika kwa sare ya bao 1-1 kati ya Dodoma Jiji na Singida Black Stars, matokeo yaliyoifanya timu hiyo kufikisha pointi 11 baada ya mechi saba.
Kilichozua mjadala ni muda mfupi ambao mshambuliaji huyo aliutumia uwanjani kabla ya kuonyeshwa kadi hiyo. Sowah aliingia dakika ya 77 akitarajiwa kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji, lakini dakika 11 baadaye alilazimika kuondoka uwanjani baada ya tukio lililomkutanisha na mchezaji wa Dodoma Jiji, Andy Bikoko.
Sowah alionyeshwa kadi hiyo kufuatia tukio la kumpiga Bikoko dakika chache baada ya kufanya faulo, kitendo kilichosababisha aonyeshwe kadi nyekundu. Tukio hilo liliibadilisha hali ya mchezo kwa Singida Black Stars, ambayo ililazimika kuendelea na dakika zilizobaki ikiwa pungufu.
Kupitia taarifa yake, klabu hiyo imesema Kamati ya nidhamu itafanya mapitio ya tukio hilo ili kutathmini mazingira yake na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa kanuni na taratibu za klabu.
Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza, alisema; “Tutalipitia tukio hili kwa kina, kuangalia mazingira yake na kuhakikisha hatua zitakazochukuliwa zinafuata kanuni na taratibu za klabu. Nidhamu ni jambo muhimu kwa kila mchezaji anayeivaa jezi ya Singida Black Stars.”
Massanza aliongeza: “Tunatambua umuhimu wa Sowah katika kikosi chetu, lakini kila mchezaji ana wajibu wa kuilinda timu na kuheshimu mchezo. Tunataka kuona wachezaji wakizingatia nidhamu na kuelekeza nguvu zao katika kusaidia timu kupata matokeo mazuri.”
Kutokana na kadi hiyo nyekundu, Singida BS itakosa huduma ya mshambuliaji huyo katika michezo miwili ijayo ya ligi dhidi ya Coastal Union, Jumanne ya Oktoba 12, 2026 na TRA United Oktoba 24, 2026.
Sowah alirejea Singida BS baada ya kuachana na Simba, klabu ambayo ilimtuhumu mshambuliaji huyo kuwa na utovu wa nidhamu.