KIUNGO Feisal Salum ‘Fei Toto’ amemfurahisha kocha Florent Ibenge baada ya kuonyesha kutokata tamaa kwa kuifungia Azam bao la ushindi, hatua iliyorejesha kikosi hicho kwenye njia ya ushindi baada ya kupoteza dhidi ya Simba.
Azam juzi ilicheza mechi ya saba dhidi ya Coastal Union na kuit andika mabao 2-0, ushindi ulioifanya iendelee kusalia nafasi ya tatu ikiwa na pointi 17.
Akizungumza na Mw anaspoti, Ibenge alisema ushindi huo ni hatua nzuri kwa timu yake, akiwapongeza wachezaji kwa kuonyesha ukomavu katika namna walivyoamua mchezo, ingawa amedai ushindi ungekuwa mkubwa zaidi kama bao la kwanza la Fei Toto lingekubaliwa baada ya kukataliwa na mfumo wa FVS.
“Ushindi huu ni hatua nzuri kwetu baada ya kupoteza dhidi ya Simba. Wachezaji wameonyesha ukomavu katika kuamua mechi, lakini sijaona tatizo kwenye bao la kwanza la Fei Toto,” alisema Ibenge.
Kocha huyo alisema jambo lililomfurahisha zaidi ni namna Fei Toto alivyoendelea kupambana licha ya bao lake la kwanza kukataliwa, kabla ya kurejea na kufunga bao la pili lililowahakikishia ushindi huo muhimu.
“Jambo zuri kuhusu Fei ni kwamba hakukata tamaa baada ya bao lake la kwanza kukataliwa. Aliendelea kupambana na kufunga tena bao la pili ambalo lilitupa ushindi,” alisema.
Azam imekuwa na matokeo yenye kupanda na kushuka msimu huu, ikianza kwa sare ya 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania, kisha kushinda dhidi ya TRA United na Pamba Jiji kwa mabao 2-1 kabla ya kupoteza 0-2 dhidi ya Simba.
Kwa upande wa Fei Toto ambaye mpaka sasa ana mabao mawili kwenye ligi, tangu atue Azam akitokea Yanga msimu wa 2023/24, amekuwa miongoni mwa wachezaji muhimu wa timu hiyo, akifunga mabao 19 katika msimu wake wa kwanza, manne msimu wa 2024/25 na 14 katika Ligi Kuu msimu wa 2025/26.
Ibenge alisema hatua inayofuata ni kwa Azam kuendeleza ushindi huo na kujenga mwendelezo mzuri wa matokeo, huku wakijiandaa kwa mchezo wao wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya ZED ya Misri mchezo utakaopigwa Oktoba 16, 2026.
“Sasa akili zetu zimeshatoka kwenye mchezo uliopita, tunaweza zaidi mechi za kimataifa na tunataka kupata ushindi katika mchezo huo wa kwanza.”
Azam ambayo msimu uliopita ilifika hatua ya makundi kwa mara ya kwanza inatakiwa kuhakikisha kuwa inafanya vizuri kutokana na ubora wa ZED ambayo imekuwa ikionyesha kiwango cha juu kwenye kila mchezo ambao imekuwa ikicheza msimu huu.