ZFF yafungua ukurasa wa soka la kidijitali
Muktasari:
- Kupitia mkataba huo, ZFF itanufaika na huduma za intaneti pamoja na Sh150 milioni kwa ajili ya shughuli zake za kiuendeshaji, huku hatua hiyo ikitarajiwa kuongeza ufanisi wa shirikisho na kuboresha namna mashabiki wanavyopata taarifa za soka.
SHIRIKISHO la Soka Zanzibar (ZFF) limefungua ukurasa mpya katika uendeshaji wa soka baada ya kuingia mkataba wa ushirikiano na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), unaolenga kuharakisha matumizi ya teknolojia katika sekta ya soka Zanzibar.
Kupitia mkataba huo, ZFF itanufaika na huduma za intaneti pamoja na Sh150 milioni kwa ajili ya shughuli zake za kiuendeshaji, huku hatua hiyo ikitarajiwa kuongeza ufanisi wa shirikisho na kuboresha namna mashabiki wanavyopata taarifa za soka.
Ushirikiano huo pia utawezesha ZFF kutumia majukwaa ya kidijitali kuwafikishia mashabiki taarifa kwa wakati, ikiwemo ratiba za mechi, matokeo, taarifa za timu na wachezaji pamoja na habari za mashindano mbalimbali yanayoendeshwa Zanzibar.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba huo, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Pembe Juma, amesema teknolojia imekuwa sehemu muhimu ya uendeshaji, ufuatiliaji na utangazaji wa michezo katika dunia ya sasa.
Amesema ushirikiano huo utasaidia soka la Zanzibar kuwafikia wananchi kwa urahisi zaidi kupitia majukwaa ya kidijitali, huku ukitoa fursa kubwa kwa vijana, wachezaji na klabu kujitangaza na kuonekana zaidi.
Pia, Waziri huyo aliipongeza ZFF kwa kuanza kutumia mfumo wa N-CARD katika uuzaji wa tiketi za kielektroniki viwanjani.
Amesema matumizi ya mfumo huo yanaweza kusaidia kuondokana na utegemezi wa tiketi za karatasi, huku yakiboresha ufanisi, usalama na udhibiti wa mapato ya michezo.
Hata hivyo, aliitaka TTCL na ZFF kuweka mpango madhubuti wa utekelezaji wa mkataba huo, ukiwa na malengo na muda maalumu wa kuyafikia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Biashara wa TTCL, Vedastus Mwita, amesema ushirikiano huo unalenga kuiwezesha ZFF kupata intaneti na suluhisho mbalimbali za kidijitali zitakazoboresha shughuli zake.