Zanzibar kutumia Afcon 2027 kutangaza utalii
Muktasari:
- Tanzania, Uganda na Kenya ndio wenyeji katika michuano hiyo itakayoanza Juni 19, 2027 hadi Julai 17, 2027, hivyo Zanzibar inatumia fursa hiyo kutangaza utalii kupitia vivutio.
KAIMU Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mudrick Ramadhan Soraga amesema Serikali imejipanga kutumia michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027 kukuza utalii kisiwani hapa.
Tanzania, Uganda na Kenya ndio wenyeji katika michuano hiyo itakayoanza Juni 19, 2027 hadi Julai 17, 2027, hivyo Zanzibar inatumia fursa hiyo kutangaza utalii kupitia vivutio.
Soraga ambaye pia ni Waziri wa Teknolojia ya Habari, Mawasiliano na Ubunifu Zanzibar, amesema sekta ya utalii imejipanga kuhakikisha wageni wote wanapatiwa huduma bora.
“Zanzibar ni miongoni mwa vituo vya michuano hiyo hivyo tutahakikisha tunatoa huduma bora kwa wageni wetu watakaofika ili kuwafanya waongeze muda wakukaa kisiwani hapa,” amesema.
Amesema kupitia michuano hiyo wataandaa matamasha mbalimbali ya utamaduni na muziki yatakayowapa wageni fursa ya kufurahia kuwepo Zanzibar. Aliongezea, viongozi wa Serikali kwa kushirikiana kwa pamoja watahakikisha matakwa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) yanatekelezwa kwa wakati.