ACT, SMZ wavutana kuhusu gharama halisi ujenzi Uwanja wa AFCON
Muktasari:
- Hatua hiyo inakuja kutokana na kuwapo kwa takwimu tatu tofauti zinazotajwa kwa nyakati na taarifa tofauti hivyo kuibua mjadala mkubwa baina ya pande hizo mbili.
Wakati Chama Cha ACT Wazalendo kikishangazwa kuwapo takwimu tofauti na kubwa kuhusu gharama za ujenzi wa uwanja utakaotumika kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Africa (AFCON) 2027, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetoa ufafanuzi huku ikionya kutaja takwimu ambazo sio sahihi kwa ajili ya kupotosha umma.
Hatua hiyo inakuja wakati kukiibuka mjadala kuhusu gharama za ujenzi wa mradi huo kukiwa na takwimu tofauti kuhusu gharama halisi ya ujenzi wa uwanja huo.
Wakati akizindua mabasi ya umeme, Julai 23, 2026, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi alionya kile alichokiita upotoshaji uliofanywa na mtu ambaye hakumtaja huku akinukuu maneno yake kwamba serikali inajenga uwanja huo kwa gharama ya Sh1.4 trilioni.
Licha ya kutokumtaja, lakini kauli hiyo ilikuwa imetolewa na Mwenyekiti wa ACT Taifa, Othman Masoud katika mahojiano maalumu na kituo cha luninga cha Wasafi Tv ambapo alisema gharama zinazotumika kujenga uwanja huo ni kubwa na haziwezi kurejeshwa.
“Tunaambiwa Serikali itatenga Sh1.6 trilioni kwa ajili ya Kijiji cha AFCON, niambie kwa Zanzibar ambao leo tuna fursa kubwa ya utalii, sekta ya utalii inahitaji vitu vingi, unakwenda kuwekeza Sh1.6 trilioni kwa ajili ya Kijiji cha AFCON, hizi fedha zitarejeshwaje?” alihoji Othman
Akizungumza hilo Dk Mwinyi alisema, “kwanza, fedha zilizotajwa si sahihi. Si kweli kwamba tunatumia Sh1.4 trilioni. Mzushi. Nikifanya mema, husemi. Kwa wasiojua, mradi wa ujenzi wa uwanja wa michezo wa kwa ajili ya mashindano ya AFCON una gharama ya dola za Kimarekani milioni 150, ambayo ni kama Sh300 bilioni, sio Sh1.4 trilioni,” alisema Dk Mwinyi.
Wakizungumza na waandishi wa habari, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanaotokana chama cha ACT Wazalendo, katika Baraza la Wawakilishi, leo Julai 29, 2026 wameitaka Serikali kutoa taarifa sahihi na kamili kwa umma na kuweka wazi juu ya tofauti zilizojitokeza katika taarifa za gharama za ujenzi wa uwanja huo.
Akisoma taarifa ya wawakilishi hao, Mnadhimu wa Chama hicho katika Baraza la wawakilishi, Profesa Omar Fakih Hamad amesema wananchi wamebaki njia panda kuwapo na takwimu tofauti za serikali.
“Kwetu sisi tumepata wasiwasi mkubwa wa utofauti wa taarifa sahihi zilizotolewa na Serikali moja. Tunataka kujua usahihi ni upi, je ni nani mkweli kati ya Rais ambaye ndiye mkuu wa nchi au Waziri wa Fedha na Mipango ambaye anafanya kazi kwa niaba ya Rais,” alisema Profesa Fakih
Kwa mujibu wa Profesa Omar Fakih, wakati wa kusomwa bajeti kuu ya SMZ ya mwaka 2026/27, Waziri wa Fedha alisema kufuatia uwepo wa mashindano ya AFCON 2027, Serikali imetenga Sh1.69 trilioni ili kuwekeza katika kuimarisha miundombinu ya AFCON.
Amesema asili ya Uwanja wa Fumba na Mji wa Michezo wa AFCON ni miradi ya uwekezaji na sio ya huduma kwa jamii na kama ni kwa huduma kwa jamii tu, Uwanja wa Amani, Uwanja wa Mao na viwanja vya kila wilaya vinatosha.
Waziri wa Fedha afafanua
Akitoa ufafanuzi kuhusu madai hayo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Juma Malik Akili amesema wanasiasa hao wana nia ya kupotosha umma kwani gharama za mradi huo zipo wazi na sio Sh1.6 trilioni kama wanavyotaja.
Kwa mujibu wa Dk Malik Bjeti Kuu ya serikali ya mwaka 2026/27 hakuna sehemu ambayo serikali iliandika au kutamka kukopa fedha Sh1.6 trilioni kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vya AFCON Fumba.
“Kitabu cha bajeti kimeandikwa na taarifa zipo kwenye Hansard kila mahali na hilo halikuwa sahihi hata kidogo kiwango kilichotajwa kwenye bajeti kuu ya serikali ni Sh1.069 trilioni kwa ajili ya uwekezaji katika miradi yote inayohusu AFCON na sio Sh1.6 trilioni kama inavyozungumzwa,” amesema
Hata hivyo baada ya Mwananchi kupitia tena kitabu cha bajeti fedha halisi zilizotajwa ni Sh1.069 trilioni.
Katika ufafanuzi wa Dk Malik akirejea ukurasa wa 98 wa kitabu cha bajeti, kinachofanywa na serikali ni kupitia miradi jumuishi ikiwemo barabara za njia sita, utalii, huduma za jamii, bandari na viwanja vya ndege kwa lengo la kutumia mashindano hayo kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi, ajira na kulitangaza taifa kimataifa.
“Bajeti tuliyoisema ni jumuishi hivyo kwa yule aliyeripoti bila ya kutaka ufafanuzi huyu amekosea na sio jambo la busara kupotosha umma,” amesema
Akizungumza kuhusu kauli ya Dk Mwinyi aliyotolea ufafanuzi wakati wa kuzindua mabasi ya umeme, Dk Malik amesema ni sahihi kwani gharama hiyo ni kwa ajili ya ujenzi wa uwanja pekee.
Waziri Malik amesema serikali ilianza ujenzi wa uwanja huo tangu bajeti ya mwaka 2025/26 na kutumia Sh165 bilioni na mwaka wa fedha 2026/27 serikali inatumia Sh186 bilioni sawa na Sh351 bilioni kwa ajili ya uwanja pekee bila miradi mingine.
Akizungumzia faida ya uwepo wa mashindano hayo amesema ni kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi, kibiashara, kiutalii, kuzidi kwa mapato ya nchi na kuendelea kuitangaza nchi kupitia mashindano hayo.
Amesema fursa nyengine ni kuvutia watu wengi kupata fursa zilizopo Tanzania ikiwemo Zanzibar na kushawishi wawekezaji wa ndani na nje, kukuza ajira kwa vijana, kukuza vibaji na ujuzi wa vijana kimichezo