Yanga yaanza na sare Mapinduzi Cup, Kaze ashusha lawama kwa waamuzi
Mechi ya kwanza kundi A ya Mapinduzi Cup 2020 yanayoendelea kufanyika Zanzibar imemalizika kwa Yanga kulazimishwa sare ya 0-0 dhidi ya Jamhuri.
Mechi hiyo iliyokuwa na burudani za kutosha baada ya pande zote kucheza kiufundi kwa mipira ya pasi na kutengeneza nafasi za mashambulizi ambayo hazikuzaa mabao.
Yanga walianza kwa kulisakama goli la Jamhuri chini ya kipa Nassir Tarib kipindi cha kwanza wakitumia mipira ya pembeni ila mshambuliaji Waziri Junior hakuwa na umakini wa kumalizia mipira aliyotengewa.
Jamhuri walifanya mashambulizi kwa kupiga mashuti langoni kwa Yanga huku golikipa Faruk Shikhalo akiwa makini kuicheza ikiwemo kuokoa mchomo uliopigwa ndani ya boksi.
Kipindi cha pili Yanga ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa wachezaji kadhaa yaliyowawezesha kufika mara kwa mara langoni mwa Jamhuri ila hawakuweza kupata bao.
Kuingia kwa Tuisila Kisinda, Michael Sarpong, Yacouba Sogne na Kibwana Shomari kuliiongezea Yanga nguvu ya kushambulia wakimtumia Kisinda kuwapunguza kasi mabeki.
Jamhuri walifanya mabadiliko ya kuongeza watu wa kuzuia na kufanya mashambulizi ya kushtukiza na kujikuta wakicheza madhambi mara kwa mara kutokana na umiliki wa mpira waliounyesha Yanga.
Kaze afunguka
Katika mahojiano na waandishi wa habari Kaze alipoulizwa kwanini hajatumia wachezaji wake wa kila siku aliwatetea kwa kusema wametumika sana katika Ligi kwa kusafiri siku 21 kwenda kucheza mechi za ligi.
"Tunaamini wachezaji waliopo Yanga wote wanaweza kucheza mashindano mbalimbali kama haya Mapinduzi, kuna wachezaji wametumika sana kwenye ligi na mwili wa mchezaji inabidi upumzike," amesema Kaze
Kaze pia amedai hakupendezwa na waamuzi hawakuwa mchezoni kwakuwa uliwazidi mbinu.
"Hilo siwezi kulizungumzia sana mimi sio wa kuzungumzia ila tutajipanga," amesema Kaze.
Kwa upande wake Kocha wa Jamhuri, Mafaume Shaaban amesema walitarajia kupata alama tatu kwa Yanga ila watajipanga kwa mechi ijayo dhidi ya Namungo kwasababu hawajawahi kucheza nao kabisa.
Alikiba atoa burudani
Baada ya dakika 45 za kipindi cha kwanza kumalizika staa wa muziki nchini Alikiba aliwa sapraizi mashabiki kwa kuingia kuwapa burudani ya muziki.
Alikiba alianza kuimba wimbo wa dodo, kisha proud of you alioshirikishwa na darassa na kumalizia na wimbo wa kadogo.
Alikiba aliimba huku akiwafuata mashabiki jukwaani na kuwaimbisha nyimbo hizo.