Yanga ya moto, Toure, Nzengeli waibeba
Muktasari:
- Ushindi huo unairudisha Yanga juu ya msimamo wa ligi, ikifikisha pointi 12 sawa na Simba, lakini bingwa mtetezi akibebwa na tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa.
YANGA imeendelea kukusanya pointi ikishinda mechi ya nne mfululizo katika Ligi Kuu Bara, baada ya leo Agosti 28, 2026 kuichapa Pamba Jiji mabao 2-0.
Ushindi huo unairudisha Yanga juu ya msimamo wa ligi, ikifikisha pointi 12 sawa na Simba, lakini bingwa mtetezi akibebwa na tofauti nzuri ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Dakika 17 tu zilitosha kwa Yanga kupata bao la kuongoza likifungwa na Maxi Nzengeli, akiitumia asisti ya mshambuliaji, Cheikh Toure.
Wakati Pamba Jiji ikijiuliza, ikaruhusu bao lingine dakika ya 22 mfungaji akiwa Toure akimalizia pasi ya Peter Shalulile.
Bao hilo linakuwa la kwanza kwa Toure akifungua akaunti yake ya mabao tangu asajiliwe na mabingwa hao msimu huu.
Yanga ikitawala vizuri mchezo huo, ingeweza kupata mabao zaidi endapo wachezaji wake wangekuwa na utulivu, ikimaliza kipindi cha kwanza na uongozi wa mabao hayo.
Kipindi cha pili mzimu wa kupoteza umakini ukaendelea kuiandama Yanga ikipoteza nafasi nyingi za kufunga.
Ndani ya mchezo huo, Yanga iliwatambulisha wachezaji wake wawili wakicheza kwa mara ya kwanza akiwemo kiungo Freddy Ngoma aliyecheza kwa dakika 74 akitolewa na kuingia Aziz Andambwile.
Mbali na Ngoma, mshambuliaji Seleman Mwalimu naye aliingia akitokea benchi, akichukua nafasi ya Toure dakika ya 64, akicheza mechi yake ya kwanza tangu asajiliwe akitokea Simba.
Kipigo cha leo, kinaifanya Pamba Jiji kupoteza mechi ya tatu kati ya nne ilizocheza ikifungwa 2-1 na Simba, kisha matokeo kama hayo mbele ya Azam. Mechi ya kwanza ilitoka sare ya 1-1 dhidi ya Dodoma Jiji.