Geita Gold yaibania Azam dakika za jioni!
Muktasari:
- Mechi hiyo iliyopigwa leo Agosti 28, 2026 kwenye Uwanja wa Bukombe uliopo mji mdogo wa Ushirombo, katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, ilishuhudia ushindani mkubwa, huku pia FVS ikiamua mabao mawili.
MATAJIRI wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC wameshindwa kutamba katika mechi ya mzunguko wa nne ya Ligi Kuu Bara, baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Geita Gold, huku teknolojia ya Football Video Support (FVS), ikiamua baadhi ya matukio.
Mechi hiyo iliyopigwa leo Agosti 28, 2026 kwenye Uwanja wa Bukombe uliopo mji mdogo wa Ushirombo, katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, ilishuhudia ushindani mkubwa, huku pia FVS ikiamua mabao mawili.
Katika mechi hiyo, Azam FC ilikuwa ni ya kwanza kupata bao la penalti ya dakika ya 45+2, iliyofungwa na Abdul Suleiman 'Sopu', baada ya beki wa Geita Gold, Haroub Abdallah kuushika mpira akiwa kwenye eneo la hatari.
Haroub alishika mpira huo uliopigwa na beki wa kulia wa Azam FC, Lusajo Mwaikenda, japo tukio hilo la utata liliamuliwa kwa teknolojia ya Football Video Support (FVS), baada ya mwamuzi wa kati, Saad Mrope wa Dodoma kushindwa kuona mwanzoni.
Wakati Azam FC ikiamini inaenda mapumziko kifua mbele, Geita Gold ilichomoa bao hilo kwa penalti pia iliyopigwa na aliyekuwa mshambuliaji wa kikosi hicho, Mzambia, Obrey Chirwa dakika ya 45+8.
Kipindi cha pili timu zote zilitengeneza mashambulizi, dakika ya 90+1, Azam FC ilipata bao la pili lililofungwa na kiungo, Himid Mao Mkami aliyepokea pasi nzuri ya beki, Twalibu Nuru na kupiga shuti lililomshinda kipa, Frank Faustine.
Hata hivyo, wakati Azam ikiamini mechi hiyo imeisha, Geita Gold ilijibu mapigo na kusawazisha bao hilo dakika ya 90+3, kupitia kwa Martin Kigi aliyetumia vizuri makosa ya kipa, Zuberi Foba aliyetokea na kuupiga mpira moja kwa moja golini.
Mpira huo ulitokana na pasi ndefu iliyopigwa na kiungo mkabaji, Abdallah Kulandana na wakati unakaribia eneo la hatari la Azam, Foba alitoka golini kwa ajili ya kuokoa, japo alishindwa kutimiza alichokusudia na kumkuta Kigi aliyepiga shuti huku golini kukiwa hakuna mtu.
Katika mechi nne ilizocheza Geita msimu huu, ilianza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City, Agosti 14, 2026, ikachapwa 1-0 na Namungo FC, Agosti 18, 2026, ikaifunga Kagera Sugar mabao 6-2, Agosti 22, 2026 na leo sare ya 2-2 mbele ya Azam FC.
Kwa upande wa Azam, ilianza kwa sare ya bao 1-1, dhidi ya Polisi Tanzania, Agosti 15, 2026, ikaifunga TRA United mabao 2-1, Agosti 20, 2026 na kuichapa pia Pamba Jiji mabao 2-1, Agosti 23, 2026, kisha leo imefungana mabao 2-2 na Geita Gold.
Kabla ya leo, mara ya mwisho timu hizi kukutana katika Ligi Kuu ilikuwa Mei 28, 2024, kwenye Uwanja wa Nyankumbu, Geita, ambapo Azam FC ilishinda mabao 2-0, yaliyofungwa na Yeison Fuentes dakika ya 58 na Feisal Salum 'Fei Toto' dakika ya 71.
Tangu Geita Gold iliposhiriki Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza msimu wa 2021-2022, haijawahi kuifunga Azam, mechi ya leo ni ya saba kwao kukutana, ambapo kati ya hizo imechapwa mara tatu, huku minne iliyobakia ikiisha kwa sare.
Katika mechi nne ilizocheza Azam FC, inafikisha pointi nane ikiwa nafasi ya nne, baada ya kushinda mechi mbili na kutoka sare mbili, huku Geita Gold ikishika ya tano na pointi saba, kufuatia kushinda mbili, ikitoa sare moja na kupoteza moja.