Yanga Princess yaanza kwa mbwembwe
Muktasari:
- Mnally aliwataka mashabiki wa Yanga Princess kuendelea kuiunga mkono timu hiyo na kutowakatia tamaa wachezaji, akisisitiza kuwa msimu ndiyo kwanza umeanza na bado wana mengi mazuri ya kuonyesha kadiri ligi inavyoendelea.
NAHODHA wa Yanga Princess, Diana Mnally amesema ushindi wa mechi mbili mfululizo ugenini umeongeza morali na motisha kwa wachezaji wa timu hiyo katika kuendeleza mapambano ya kusaka matokeo mazuri kwenye Ligi Kuu ya Wanawake.
Yanga Princess imeanza msimu wa 2026/27 kwa mafanikio baada ya kukusanya pointi sita katika michezo miwili ya ugenini. Ilianza kwa kuichapa Bunda Girls mabao 3-0, kabla ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Geita Queens katika mchezo wa pili.
Matokeo hayo yameifanya timu hiyo kufikisha pointi sita na kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi. Mnally amesema huo ni mwanzo mzuri ambao wanapaswa kuendeleza katika michezo ijayo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutimiza malengo yao msimu huu.
Akizungumzia ushindi dhidi ya Geita Queens, Mnally amesema matokeo hayo ni muhimu kwa sababu yameiwezesha timu kuendeleza wimbi la ushindi. Ameongeza kuwa kupoteza mchezo huo kungewaweka katika mazingira magumu zaidi ya kutafuta matokeo mazuri kwenye mechi zinazofuata.
“Ni alama nzuri kwa mchezo unaofuata, kwa sababu tungepoteza mechi hii ingekuwa ngumu, sababu unatoka kupoteza halafu unatafuta na timu nyingine kwa nguvu,” amesema nahodha huyo.
Mnally aliwataka mashabiki wa Yanga Princess kuendelea kuiunga mkono timu hiyo na kutowakatia tamaa wachezaji, akisisitiza kuwa msimu ndiyo kwanza umeanza na bado wana mengi mazuri ya kuonyesha kadiri ligi inavyoendelea.
“Mashabiki waendelee kutusapoti, wasitukatie tamaa, ndiyo kwanza msimu umeanza. Ninaamini kuna vitu vizuri vinakuja mbele.”