Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga hii inakamatika kabisa, Ashanti ni matatizo makubwa

Muktasari:

  • Yanga bado wameendelea kuwa na tatizo la kufanya mashambulizi yao yote kupitia winga ya kulia wakimtumia zaidi Saimon Msuva jambo ambalo ni hatari kwa timu zenye mwalimu mjanja kidogo tu. Inakamatika kama ikipata mpinzani mjanja.

NILIKUWA kwenye Uwanja wa Taifa Jumamosi iliuopita kwa mambo mawili. Kwanza ni kushuhudia mechi ya kwanza ya msimu mpya kwenye Uwanja huo na pili ni kuangalia uwezo wa Yanga na Ashanti mpya. Lakini baadaye matokeo ya ushindi wa mabao 5-1 iliyopata Yanga hayakunishangaza sana.

Hii ni kutokana na aina ya mchezo niliouona. Yanga ambao ni mabingwa watetezi walitumia mfumo wa 4-4-2 ambao si mzuri endapo watakutana na timu inayotumia mfumo wa 4-3-3. Mfumo huo unawafanya muda wote wasiwe na mtu wa mwisho na katika mechi yao na Ashanti kiwango cha mabeki Nadir Haroub ‘Canavaro’ na Mbuyu Twite hakikuwa vizuri kiasi cha kufanya makosa mengi, umakini finyu wa mastraika wa Ashanti ndio uliowaponza.

Yanga bado wameendelea kuwa na tatizo la kufanya mashambulizi yao yote kupitia winga ya kulia wakimtumia zaidi Saimon Msuva jambo ambalo ni hatari kwa timu zenye mwalimu mjanja kidogo tu. Inakamatika kama ikipata mpinzani mjanja.

Sehemu ya kati ambayo ina Athuman Idd Chuji, Haruna Niyonzima, Salum Telela na Msuva inacheza kizamani. Niyonzima dakika zote yupo kushoto jambo ambalo ni hatari kama mmoja wao atadhibitiwa ndio timu imekufa. Jerry Tegete ni mwoga kucheza kwenye nafasi yake ya straika na matokeo yake muda mwingi anamuacha Didier Kavumbagu.

Mabao yote Yanga inayafunga kupitia pembeni, timu haina mpango mbadala ‘plan B’. Isipobadilika itapata wakati mgumu sana kwenye mechi ya Coastal Union kesho Jumatano.

Turudi kwa Ashanti. Ina matatizo makubwa. Kwanza wachezaji wake hawajajengwa kisaikolojia kujua kwamba sasa wako katika ligi nyingine kubwa zaidi ya ile waliyotoka. Pili ni lazima wajitambue kuwa wanatakiwa wawe wazuri ndani ya uwanja bila kujali imani kubwa waliyonayo wapenzi wao kwao.

Uzoefu mdogo wa baadhi ya wachezaji wao ndio kwa kiasi kikubwa umechangia kuvurugwa na Yanga na wasiposhituka sasa bado kuna vipigo vingi mbele yao. Kipa Ibrahim Abdallah alishindwa kucheza kwenye nafasi yake, hajui nini cha kufanya na kwa wakati gani.  Tegete alimfunga kwa sababu hiyo, goli la Msuva pamoja na la Niyonzima ukiacha lile la Nizar pia hivyo hivyo.

Mabeki wa kati Tumba Sued na Ramadhani Malima hawajiamini, mabeki wa pembeni wa Ashanti hasa yule Emmanuel Kichiba ni kijana mdogo lakini ana uwezo kilichokosekana kwake ni mtu wa kumjenga kisaikolojia kuwa anacheza na timu ya aina gani matokeo yake alipata kadi mbili za uzembe kabisa huku benchi likiwa kimya.

Beki wa kulia ambaye ni mzoefu kidogo na alikuwa nahodha Khan Simba ni huruma tu ya Mwamuzi Israel Nkongo lakini alitakiwa kutokuwepo uwanjani mapema baada ya kuwa anacheza rafu ambazo hata faida hazina na wakati akijua kabisa ana kadi ya njano.

Viungo wa kati wakiongozwa na Emmanuel Memba, Mussa Nampaka, Joseph Mahundi na Fakihi walicheza vizuri dakika 20 tu za mwanzo baada ya hapo hawakuonekana tena, kitaalamu walikuja na nguvu mno wakati hiyo nguvu hawana, upo uwezekano wa kuwa walifanya mazoezi ya nguvu mno kwa ajili ya mechi hii na si kwa ajili ya ligi .

Mastraika wa Ashanti kipindi cha kwanza hawakuwa makini na haswa Mussa Kanyaga alikuwa mzito kuamua. Hussein Sued uzoefu wake uliwasumbua mabeki wa kati wa Yanga kiasi cha Cannavaro kuonekana anapwaya kiasi cha kuwa na mashaka naye kuwa huenda Kelvin Yondani ndio anayemfichia makosa yake.

Kimsingi Ashanti ni lazima watambue wameingia katika ligi nyingine kabisa na si sehemu ya kubahatisha na kwamba ujuaji mwingi unaweza ukawafanya kama vile wako katika daraja la Manzese unapandia kushoto unashukia kulia.

Makocha bado wana kazi ya kufanya kuwajenga wachezaji kisaikolojia.

Mwandishi wa makala hii ni Kocha wa zamani wa Yanga na Ashanti, sasa ni mfanyakazi wa Mamlaka ya Bandari na mchambuzi wa soka.