Mpanzu atia timu Kigali
Muktasari:
- Awali, kulikuwa na wasiwasi kuhusu safari ya nyota huyo kutokana na tahadhari zilizowekwa kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika baadhi ya maeneo ya DR Congo, hali iliyozua hofu kuwa angechelewa kujiunga na kikosi.
KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Elie Mpanzu, amewasili usiku wa kuamkia leo mjini Kigali, Rwanda na kuungana na wenzake wanaoendelea na maandalizi ya msimu mpya kupitia mashindano ya Kombe la CECAFA Kagame.
Awali, kulikuwa na wasiwasi kuhusu safari ya nyota huyo kutokana na tahadhari zilizowekwa kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika baadhi ya maeneo ya DR Congo, hali iliyozua hofu kuwa angechelewa kujiunga na kikosi.
Hata hivyo, Mpanzu amefanikiwa kutua Kigali na kuondoa hofu hiyo, huku Simba ikithibitisha kuwasili kwake kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Klabu hiyo imeposti video ikimuonyesha Mpanzu akiwa kambini, ambapo alitoa salamu fupi kwa mashabiki akimwambia msimamizi wa mitandao wa Simba.
"Waambie Wanasimba nipo Kigali," kauli ambayo imewafurahisha mashabiki waliokuwa wakisubiri kuungana kwake na kikosi.
Mpanzu anatarajiwa kushuhudia mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi wa CECAFA Kagame kati ya Simba na Singida Black Stars utakaochezwa leo kwenye Uwanja wa Amahoro kabla ya kuanza mazoezi na wenzake kesho kwenye Uwanja wa FERWAFA.
Ujio wake unaongeza nguvu kwenye kikosi cha Simba wakati benchi la ufundi likiendelea kukamilisha maandalizi kuelekea Simba Day, Ngao ya Jamii na msimu mpya wa mashindano ya ndani na kimataifa.