Wawili wategwa Azam FC
Muktasari:
- Diakite aliyejiunga na timu hiyo Julai 16, 2024, akitokea AS Real Bamako ya kwao Mali, amekosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza mara kwa mara, jambo linalomweka hatarini ya kuondoka, licha ya kubakisha mkataba wa mwaka mmoja hadi 2028.
KIKOSI cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC kimetua jijini Kigali, Rwanda kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa 2026-2027, huku nyota wawili wa kikosi hicho ambao ni beki, Landry Zouzou na winga, Cheickna Diakite wakiwekwa mtegoni.
Diakite aliyejiunga na timu hiyo Julai 16, 2024, akitokea AS Real Bamako ya kwao Mali, amekosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza mara kwa mara, jambo linalomweka hatarini ya kuondoka, licha ya kubakisha mkataba wa mwaka mmoja hadi 2028.
Usajili wa Kipre Junior aliyerejea tena Azam FC akitokea MC Algiers ya Algeria, Hassan Mubiru kutokea SC Villa ya kwao Uganda na Mkongomani Henoc Molia aliyetoka FC Saint-Eloi Lupopo, unaiweka nafasi finyu kwa Diakite kubaki tena kikosini.
Kwa upande wa beki wa kati mwenye uwezo wa kucheza pia beki wa kushoto, Zouzou aliyejiunga na timu hiyo Januari 1, 2025, akitokea AFAD Plateau ya kwao Ivory Coast, licha ya kubakisha mkataba hadi mwaka 2028, ila kuna uwezekano akaachwa pia.
Zouzou aliyewahi kuichezea pia ASEC Mimosas ya kwao Ivory Coast, nafasi yake Azam FC ni ndogo, baada ya usajili wa beki wa kigeni wa kushoto, Taiwo Abdulrafiu aliyetokea Rivers United FC ya kwao Nigeria, jambo litakalochangia pia kuondoka.
Mbali na hilo, ila usajili wa mabeki wa kati, Henri Braham Stanic raia wa Ubelgiji aliyetokea Stellenbosch FC ya Afrika Kusini na Lupini Dieumerci aliyesajiliwa akitokea AS Maniema Union ya kwao DR Congo ni sababu nyingine inayoweza kumtoa.