Ndemla atua anga za Kagera Sugar
Muktasari:
- Ndemla anayemudu kucheza kiungo wa kati kwa ufasaha, anadaiwa kufikia makubaliano ya awali kujiunga na kikosi hicho cha ‘Wanankurukumbi’.
BAADA ya Kagera Sugar kupanda Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2026-2027, mabosi wanasuka upya kikosi na sasa wako katika hatua za mwisho kumsajili kiungo mkabaji wa zamani wa JKT Tanzania, Said Ndemla.
Ndemla anayemudu kucheza kiungo wa kati kwa ufasaha, anadaiwa kufikia makubaliano ya awali kujiunga na kikosi hicho cha ‘Wanankurukumbi’.
Nyota huyo aliyejiunga rasmi na JKT Tanzania, Julai 24, 2023, akitokea Fountain Gate, amemaliza mkataba na timu hiyo ya maafande, jambo lililoivutia Kagera Sugar kuanza mazungumzo ya kuipata saini yake, licha ya klabu mbalimbali kumuhitaji.
Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa Kagera Sugar, Bernard Samson Sikira alisema suala nzima la usajili limeanza tayari, japo utambulisho wa nyota wapya watakaokitumikia kikosi hicho kwa msimu wa 2026-2027, litaanza siku za hivi karibuni.
Licha ya kauli ya Sikira, ila Mwanaspoti linatambua Ndemla yupo katika hatua za mwisho za kujiunga na timu hiyo, akiendakuungana na nyota wengine wapya, wakiwemo beki wa kulia, Dickson Mhilu na kiungo, Daudi Milandu waliotokea Dodoma Jiji.
Nyota wengine ni beki wa kushoto anayecheza pia beki wa kati, Boniface Onyango kutoka Kakamega Homeboyz, mshambuliaji, Collins Maina aliyetoka Fortune Sacco FC wote Wakenya na Naku James anayecheza mshambuliaji akitokea Polisi Tanzania.