Mbisa yupo kwenye rada za Dodoma Jiji
Muktasari:
- Kipa huyo aliyemaliza na clean sheets nane za Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-2026, yupo katika mazungumzo ya kujiunga na Dodoma Jiji, akiwa mbadala sahihi wa Daniel Mgore aliyeondoka kwenye kikosi hicho baada ya mkataba wake kumalizika.
MABOSI wa Dodoma Jiji wako katika hatua za mwisho za kuipata saini ya aliyekuwa kipa namba moja wa maafande wa Tanzania Prisons, Mussa Mbisa, baada ya kumaliza mkataba na timu hiyo, iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara hadi Championship.
Kipa huyo aliyemaliza na clean sheets nane za Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-2026, yupo katika mazungumzo ya kujiunga na Dodoma Jiji, akiwa mbadala sahihi wa Daniel Mgore aliyeondoka kwenye kikosi hicho baada ya mkataba wake kumalizika.
Mgore aliyemaliza na clean sheets sita za Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-2026, ameondoka katika kikosi hicho baada ya mkataba wake kumalizika, ambapo kwa sasa yupo katika hatua za mwisho za kujiunga na TRA United kwa msimu wa 2026-2027.
Kuondoka kwa Mgore kumewafanya mabosi wa timu hiyo kuingia sokoni kwa ajili ya kutafuta kipa mwingine atakayesaidiana na Ally Salim, huku Mbisa akiwa ni chaguo muhimu kutokana na kiwango bora alichokionyesha, licha ya Prisons kushuka daraja.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa Dodoma Jiji, Fortunatus Johnson alisema wachezaji wapya waliofikia makubaliano wameanza kuwatangaza, hivyo, mchakato wa kuwasajili wengine unaendelea na utapokamilika wataweka wazi kama wanavyofanya.
Mbisa aliyewahi kucheza pia Mwadui ambayo kwa sasa ni Bigman FC, alijiunga na Prisons kwa ajili ya msimu wa 2022-2023 wa Ligi Kuu Bara, baada ya kuachana na Coastal Union, akiwa ni miongoni kwa makipa bora wazawa kutokana na kiwango chake.
Ikiwa dili hilo litakamilika, Mbisa ataungana na beki wa kulia, Marco Mhilu aliyejiunga na Dodoma Jiji akitokea Prisons, beki wa kati, Mukrim Issa ‘Miranda’ aliyetokea Singida Black Stars na mshambuliaji, Daruweshi Saliboko aliyetoka KMC FC.