Watano wapya waipa jeuri Mbeya City
Muktasari:
- Msimu uliopita timu hiyo haikuwa na matokeo mazuri hadi kusubiri matokeo ya mwisho ya mchujo ‘play off’ kufanikiwa kubaki salama Ligi Kuu na sasa inajiandaa upya na msimu ujao unaoanza Agosti 14, 2026.
WAKATI Mbeya City ikiweka kambi yake Mwakaleli wilayani Rungwe mkoani Mbeya na mastaa wake wapya watano, uongozi wa timu hiyo umetamba msimnu ujao kufanya kweli ili kurejesha furaha kwa mashabiki.
Msimu uliopita timu hiyo haikuwa na matokeo mazuri hadi kusubiri matokeo ya mwisho ya mchujo ‘play off’ kufanikiwa kubaki salama Ligi Kuu na sasa inajiandaa upya na msimu ujao unaoanza Agosti 14, 2026.
Mbeya City inatarajia kuanzia nyumbani kwa mechi tatu mfululizo ikiwaleta Sokoine Geita Gold, Dodoma Jiji na Mashujaa kisha kutoka nje dhidi ya Fountain Gate, TRA United na Polisi Tanzania.
Wachezaji ambao tayari wametambulishwa kuitumikia timu hiyo ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya ni Ismail Aziz, George Chota (pichani juu), Oscar Mwajanga, Hassan Hajji na Nassor Mbarouk, huku mazungumzo na nyota wengine yakiendelea.
Ofisa Habari wa timu hiyo, Gwamaka Mwankota, ameliambia Mwanaspoti kuwa wameanza kambi chini ya Kocha Salum Mayanga kuisuka upya Mbeya City ili kuhakikisha msimu ujao wanafanya vizuri.
Alisema msimu ujao hawataki kuona presha ikijirudia kwani ugumu na ubora wa ligi ndio unawapa hamasa kujisahihisha makosa yaliyoonekana msimu uliopita, hivyo watarudi kibabe na kuwapa raha mashabiki.
“Maumivu yalikuwa mengi kwa mashabiki msimu uliopita, tutasajili kwa ubora ili timu iwe yenye ushindani, tayari tumeachana na Kipa Beno Kakolanya na wengine tunamalizia makubaliano tuachane nao.
“Tunasajili kulingana na mahitaji ya timu kupitia mapendekezo ya Kocha, tunaamini kambi yetu huko Rungwe itakuwa na matokeo mazuri kwakuwa historia inajieleza tunapokuwa huko,” alisema Mwankota.