Wanaowania uongozi TFF waanikwa, sita wautaka urais

Muktasari:
- Taarifa iliyotolewa leo Juni 24, 2025 na Makamu Mwenyekiti Kamati ya Uchaguzi TFF, Wakili Benjamin Kalume, imetaja wagombea sita wa nafasi za urais na 19 upande wa ujumbe kamati ya utendaji.
KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetoa orodha ya awali ya waliochukua na kurudisha fomu kuomba uongozi katika Shirikisho hilo kwa ajili ya usaili utakaofanyika Julai 2 na 3, 2025 jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa leo Juni 24, 2025 na Makamu Mwenyekiti Kamati ya Uchaguzi TFF, Wakili Benjamin Kalume, imetaja wagombea sita wa nafasi za urais na 19 upande wa ujumbe kamati ya utendaji.
Hiyo inakuja baada ya Juni 21 hadi 23, 2025 kufanyika kikao cha mchujo wa awali wa wagombea na kuandika barua za kuwajulisha wagombea juu ya mchujo wa awali.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nafasi ya Urais kuna wagombea sita ambao ni Ally Mayay Tembele, Ally Thabit Mbingo, Mbette Mshindo Msolla, Mustapha Salumu Himba, Shija Richard Shija na Wallace John Karia ambaye anatetea nafasi yake.
Upande wa wajumbe kamati ya utendaji, kuna wagombea 19 kutoka kanda tofauti ambao ni CPA Hosseah Hopaje Lugano (Kanda Namba Moja), Cyprian Charles Kuyava (Kanda Namba Tatu), Evance Gerald Mgeusa (Kanda Namba Tatu), Issa Mrisho Bukuku (Kanda Namba Sita), James Patrick Mhagama (Kanda Namba Tatu), Khalid Abdallah Mohamed (Kanda Namba Mbili), Lameck Nyambaya (Kanda Namba Moja), Martin Kibua Sekisasa (Kanda Namba Mbili) na Mohamed Omar Aden (Kanda Namba Nne).
Wengine ni Ally Omary Msigwa, DR David Cleopa Msuya, DR Yono Stanley Kevela, Juvenalius Pius Rugambwa, Maanya Juma Maanya, Robert Bundala Kajuba, Rocky Raymund Mgeju, Saleh Alawi Abdulllah, Salum Alli Kulunge na Vedastus Kalwizira Lufano.
Katika uchaguzi huo utakaofanyika Agosti 16, 2025 jijini Tanga, wapiga kura watatoka kwenye kanda sita kisoka ambazo ni Kanda Namba Moja inayohusisha mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Morogoro na Pwani, huku Kanda Namba Mbili ni mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga, wakati Kanda Namba Tatu ikiwa na mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe, Ruvuma na Songwe.
Kwa upande wa Kanda Namba Nne ni mikoa ya Dodoma, Simiyu na Singida ilhali Kanda Namba Tano ina mikoa ya Geita, Mara, Mwanza na Kagera. Pia Kanda Namba Sita ina mikoa ya Katavi, Kigoma, Rukwa na Tabora.
Kwenye uchaguzi huo kuna nafasi saba zinazowaniwa ikiwamo moja ya urais na sita za wajumbe wa Kamati ya Utendaji ambapo zoezi la uchukuaji na urudishaji fomu lilianza Juni 16, 2025 na kuhitimishwa Juni 20, 2025.
Kanuni ya Uchaguzi ya Mwaka 2021 Ibara ya 10 (3 -4) inaeleza kuwa mgombea wa urais wa TFF lazima awe na barua tano za udhamini kutoka kwa wanachama wa TFF, huku kwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji kutoka kanda lazima awe na barua ya udhamini kutoka chama cha soka cha mkoa husika.
Inaongeza kuwa, mwanachama hapaswi kumdhamini mgombea zaidi ya mmoja kwa nafasi moja vinginevyo udhamini wote utakuwa batili.
Kwa mujibu wa kanuni hiyo wanaotoa uidhinishaji kwa wagombea ni 47 ambao mchanganuo wake upo hivi; vyama vya soka vya mikoa (FA) vyenye wajumbe 26, klabu za Ligi Kuu Bara (16), huku Chama wa Waamuzi Tanzania (FRAT), Chama cha Makocha Tanzania (TAFCA), Chama cha Madaktari wa Michezo (TSMA), Chama cha Wachezaji (SPUTANZA) na Chama cha Soka la Wanawake (TWFA) kila kimoja kikiwa na mjumbe mmoja.
Ratiba ya uchaguzi huo inaonesha baada ya zoezi la kuchapisha na kubandika kwenye mbao za matangazo orodha ya awali ya wagombea, kuanzia Juni 26 hadi 28 mwaka huu saa 10 jioni ni kipindi cha kupokea na kuweka pingamizi kwa wagombea.