Wamalawi wa Simba CAF wamepania
Muktasari:
- Mighty Wanderers ya Malawi, itakutana na Simba katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2026-2027, baada ya droo iliyofanyika Alhamisi iliyopita huko Cairo, Misri.
KOCHA Mkuu wa Mighty Wanderers, Bob Mpinganjira, amesema droo ngumu ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Simba SC ni fursa kwa timu yake kuonyesha maendeleo iliyofanya katika mashindano ya kimataifa.
Mighty Wanderers ya Malawi, itakutana na Simba katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2026-2027, baada ya droo iliyofanyika Alhamisi iliyopita huko Cairo, Misri.
Mabingwa hao wa Malawi watacheza mchezo wa kwanza nyumbani kati ya Septemba 4 na 6, kabla ya kusafiri kutua Tanzania kwa ajili ya mchezo wa marudiano utakaochezwa kati ya Septemba 11 na 13.
“Kwetu hii ni fursa. Ninaamini tuna uwezo wa kushindana,” amesema Mpinganjira. “Msimu uliopita hatukufanya vizuri katika Kombe la Shirikisho la CAF. Ninaamini tulijifunza kutokana na kampeni hiyo na tunapaswa kutumia mafunzo hayo kuboresha.”
Nahodha wa timu hiyo, Emmanuel Nyirenda, amesema kikosi kiko tayari kwa changamoto hiyo.
“Kila kitu kinawezekana katika soka. Nitawahamasisha wachezaji wenzangu kufanya kazi kwa bidii zaidi ili tufanye vizuri mwaka huu,” amesema.
Mshindi baina ya wawili hao, ataingia hatua inayofuata kuwania kufuzu makundi kwa kucheza na mshindi kati ya 15 de Agosto na Fomboni de Moheli.
Mchambuzi wa michezo nchini Malawi, Twaha Chimuka, amesema Wanderers itahitaji kucheza kwa kiwango cha juu ili kuiondoa Simba SC.
“Wanderers bado ina kazi kubwa ya kufanya. Kuifunga klabu kubwa kama Simba hakutakuwa jambo rahisi,” amesema.
Msimu uliopita, Simba iliishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikikamata nafasi ya mwisho kundi D ikikusanya pointi tano zilizotokana na kucheza mechi sita, ikishinda moja, sare mbili na kupoteza tatu.
Hatua ya awali, Simba iliiondosha Gaborone United kwa jumla ya mabao 2-1, kisha hatua ya pili ikaitoa Nsingizini Hotspurs ya Eswatini kwa jumla ya mabao 3-0.
Mighty Wanderers, msimu uliopita ilishiriki Kombe la Shirikisho Afrika, ikaishia hatua ya awali kwa kufungwa na Jwaneng Galaxy ya Botswana penalti 6-5, kufuatia sare ya jumla 1-1.