Wadau wamlilia Kocha Guliti
Muktasari:
- Kocha Guliti alifariki dunia Jumamosi Agosti 1, 2026 katika Hospitali ya Chumbuni, kisiwani Unguja na kuzikwa siku hiyohiyo kijijini kwao Mbalungini, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
KUFUATIA kifo cha Kocha Khamis Aman Khamis maarufu Guliti, wadau mbalimbali visiwani Zanzibar wakiongozwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), wametuma salamu zao za pole.
Kocha Guliti alifariki dunia Jumamosi Agosti 1, 2026 katika Hospitali ya Chumbuni, kisiwani Unguja na kuzikwa siku hiyohiyo kijijini kwao Mbalungini, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa watu wake wa karibu, Guliti alianguka ghafla asubuhi akiwa mazoezini na timu ya Muembe Makumbi City na kuwahishwa hospitalini, ndipo umauti ulipomkuta.
Katika salamu zake za pole, Rais wa ZFF, Dk Suleiman Mahmoud Jabir amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa hiyo, hivyo ametoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na wadau wote wa mpira wa miguu visiwani Zanzibar.
Kwa upande wa uongozi na JKU, nao umetoa pole kwa familia na kuelezea kocha huyo atakumbukwa kwa mchango wake katika kuendeleza soka, kujituma kwake, uongozi na malezi kwa wachezaji.
Pia, uongozi wa Black Sailors umesema wanaungana na familia pamoja na benchi la Muembe Makumbi katika kipindi hiki cha majonzi.
Timu zingine zilizotoa salamu za pole ni Mlandege, Uhamiaji, Sebleni United, Raskazone huku zote zikibainisha zinaungana na familia katika kipindi hiki kigumu.
Guliti enzi za uhai wake, amewahi kufundisha timu za madaraja mbalimbali ikiwemo JKU, Uhamiaji, Mlandege, Muembe Makumbi, Mapembeani na Kundemba zote za Zanzibar. Pia Stand United na Mbao za Tanzania Bara.
Pia kocha huyo amewahi kuhudumu katika timu za taifa za vijana Zanzibar ikiwemo Karume Boys (U-15) iliyobeba ubingwa wa CECAFA nchini Uganda mwaka 2023.
Mbali ya kuwa kocha, pia marehemu Guliti amewahi kuwa kiongozi wa soka la vijana Wilaya ya Mjini mwaka 2018.