Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zanzibar na bajeti Sh1 trilioni AFCON 2027

ZNZ Pict

Muktasari:

  • Hayo yalibainishwa Juni 11, 2026 na Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Juma Malik Akil, wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali mwaka wa fedha 2026-2027 katika Baraza la Wawakilishi, Chukwani, kisiwani Unguja.

WAKATI Tanzania, Kenya na Uganda zikiwa wenyeji wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imetenga Sh1 trilioni za maandalizi ya michuano hiyo.

Hayo yalibainishwa Juni 11, 2026 na Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Juma Malik Akil, wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali mwaka wa fedha 2026-2027 katika Baraza la Wawakilishi, Chukwani, kisiwani Unguja.

Waziri huyo alisema kati ya fedha hizo, Sh669.754 bilioni zimeelekezwa kwenye utekelezaji na uwekezaji wa miundombinu na huduma mbalimbali kwa ajili ya maandalizi ya michuano hiyo ya kimataifa.

Alieleza, maeneo yatakayopatiwa kipaumbele ni pamoja na usafiri, miundombinu, huduma za utalii na huduma za kijamii, kwa lengo la kuhakikisha nchi inanufaika na fursa zitakazotokana na mashindano hayo.

ZN 01

“Kutokana na fursa ya uwepo wa mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2027 (Afcon), Serikali imetenga kiasi cha Sh1 trilioni kwa ajili ya uwekezaji na kuimarisha maandalizi ya kitaifa katika miundombinu ya michezo, usafiri, utalii na huduma za kijamii,” alisema.

Alisema Serikali inalenga kutumia mashindano hayo kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira kwa wananchi na kulitangaza Taifa katika jukwaa la kimataifa kutokana na sekta ya michezo.

Waziri huyo alisisitiza uwekezaji unaofanyika kwa ajili ya mashindano hayo utaacha manufaa ya muda mrefu kwa wananchi, hususan katika kuboresha miundombinu, kuimarisha huduma za kijamii na kukuza sekta ya utalii.

Dk Juma alisema Afcon 2027 inatarajiwa kuwa miongoni mwa matukio makubwa ya michezo barani Afrika, huku maandalizi yakilenga kuhakikisha Tanzania inanufaika kiuchumi na fursa zinazotokana na mashindano hayo.

ZN 02

Hivi karibuni wakati wa bonanza la michezo lililowashirikisha wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wanamichezo wa klabu ya wazee ya Arusha, Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Ali Abdulgulam Hussein alisema wizara hiyo imetenga Sh5 bilioni kwa ajili ya michuano ya Afcon, hivyo kwa sasa kiwango kimeongezeka.

Naibu huyo alisema hatua hiyo inatarajiwa kuleta manufaa makubwa ya kiuchumi na kijamii, ndiyo maana Serikali imeamua kuwekeza.

Zanzibar imeshuhudiwa kuwa na maandalizi makubwa ya mashindano kwa kuboresha miundombinu ya barabara, ujenzi wa viwanja vya mpira na kuandaa laini maalumu ya umeme itakayounganishwa na mji wa Afcon.

Serikali ya Zanzibar imeendelea kuonesha utayari wake kupokea ugeni huo kwa kuanzisha mradi wa michezo uliopewa jina la Afcon City.

Mradi huo unaojengwa Fumba kisiwani Unguja, unatarajiwa kugharimu dola za Marekani milioni 150 sawa na Sh388.8 bilioni za Tanzania ambao unalenga kuvutia watalii watakaoshuhudia mashindano hayo.

ZN 03

Katika mradu huo, kuna uwanja unajengwa unaokadiriwa kuwa na uwezo wa kuchukua watazamaji 35,000 ukiwa na viwango vya ubora vinavyokubalika na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).

April 14, 2026, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, alitembelea mradi wa Mji wa Afcon unaojengwa na kampuni ya Orkum Group ya Uturuki ambao utakuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya fainali za mashindano hayo.

Pia, Dk Mwinyi alitembelea na kukagua miundombinu inayotarajiwa kujengwa, ikiwemo hospitali, barabara, migahawa, maduka makubwa pamoja na huduma nyingine zitakazozunguka mji huo wa kisasa.

Katika ziara hiyo, Dk Mwinyi alisema maeneo hayo yatatumika kwa biashara na huduma nyingine zitakazochochea ukuaji uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

“Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji miradi hii ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika kimataifa,” alisema Dk Mwinyi.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco), Haji Haji alisema Serikali ina mpango wa kujenga laini maalumu kutoka Mtoni hadi Mji wa Afcon kuondosha, ili kuondosha changamoto ya umeme kwenye Mji huo.

ZN 04

WADAU WATIA NENO

Baadhi ya wadau wa michezo Zanzibar wametoa maoni yao kuhusiana na uwekezaji unaofanywa na Serikali kuelekea mashindano hayo Afrika.

Idrisa Yakuti alisema lengo kuu la uwekezaji huo kwa serikali ni kuitangaza nchi kimataifa na kuimarisha sekta ya utalii nchini.

Vilevile alisema hiyo ni miongoni mwa kichocheo kikubwa cha harakati ya Zanzibar kupata uwanachama wa CAF na Fifa kama jambo ambalo ndiyo kilio kikubwa kwa wadau wa michezo.

“Nafikiria hii itakuwa chachu ya kweli kwenye harakati ya Zanzibar kupata uwanachama wa CAF na Fifa,” alisema Yakuti.

Yakuti alisema bado serikali ipo katika majaribio ya kuzipambania nafasi hizo huku akiamini ipo siku itafanikiwa kama ilivyo matarajio ya wengi.

Naye Abdul Saleh alisema bajeti ya mwaka wa fedha 2026-2027 imeonesha namna Serikali inavyotoa kipaumbele kwenye sekta ya michezo. Vilevile alisema anaamini kuwa Ligi Kuu ya Zanzibar na timu zinazoshiriki zitapata nafasi ya kujifunza vitu vya kuiendeleza ligi hiyo.

Alisema hizo zote ni juhudi za kuutangaza mpira wa Zanzibar kimataifa kupitia mashindano hayo yatatoa mwelekeo na hamasa kwa timu kufanya vizuri zinapopata nafasi.

Kwa upande wa Suleiman Mohamed, alisema Serikali inapaswa kupewa pongezi kwa hatua kubwa iliyofikia hususan kwa kujenga viwanja vya mpira kukuza vipaji vya vijana.

Sambamba na hilo ni jambo la kifahari la kujivunia kuwa wenyeji wa mashindano makubwa ya aina hiyo, hali inadhihirisha kuwa Serikali inathamini michezo ndiyo maana inawekeza fedha nyingi.