Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waamuzi 53 kazini Ligi Kuu Zanzibar

WAAMUZI Pict

Muktasari:

  • Katika orodha hiyo, wapo waamuzi 21 wa kati na 32 wasaidizi, ambao watagawanywa kusimamia mechi zitakazochezwa Unguja na Pemba.

WAAMUZI 53 wamepewa jukumu la kusimamia mechi za Ligi Kuu Zanzibar msimu wa 2026/27, huku Kamati ya Waamuzi ikilenga kuhakikisha ushindani huo unaendeshwa kwa kuzingatia sheria na kanuni za soka.

Katika orodha hiyo, wapo waamuzi 21 wa kati na 32 wasaidizi, ambao watagawanywa kusimamia mechi zitakazochezwa Unguja na Pemba.

Kwa mujibu wa Kamati ya Waamuzi, ligi hiyo iliyoanza Agosti 29, 2026, itakuwa na waamuzi 14 wa kati na wasaidizi 20 kwa mechi zitakazochezwa Unguja. Kwa upande wa Pemba, waamuzi wa kati watakuwa saba, huku wasaidizi wakiwa 12.

Katibu wa Kamati ya Waamuzi, Issa Haji Vuai, amesema waamuzi hao wameandaliwa kuhakikisha michezo ya Ligi Kuu Zanzibar inachezeshwa kwa ufanisi na viwango vinavyotakiwa.

Vuai amesema miongoni mwa waamuzi hao wapo 10 waliopandishwa daraja baada ya kufaulu mtihani wa utimamu wa mwili.

“Kati ya hao, 10 wamepanda daraja na kuingia ngazi ya Ligi Kuu baada ya kufaulu mtihani wa utimamu wa mwili. Watano ni waamuzi wa kati na watano ni wasaidizi,” amesema.

Amesema kati ya waamuzi hao wapya, watatu watachezesha Unguja na saba Pemba, hatua ambayo inalenga kuongeza idadi ya waamuzi wenye uwezo wa kusimamia mechi za kiwango cha juu.

Vuai amesema mgawanyo huo ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha vipaji vya uamuzi kutoka pande zote mbili za Zanzibar vinapata nafasi ya kukua na kushiriki mashindano ya ngazi za juu.

Amesema kupandishwa kwa waamuzi hao ni hatua muhimu katika kuongeza idadi na kuimarisha kundi la waamuzi watakaosaidia kusimamia maendeleo ya soka Zanzibar.

“Uamuzi huu unalenga kutoa nafasi kwa vipaji vya uamuzi kutoka kila upande wa Zanzibar kushiriki mashindano ya ngazi za juu,” amesema.

Kwa kuanza kwa msimu mpya, macho sasa yanaelekezwa pia kwa waamuzi hao 53, ambao jukumu lao litakuwa kuhakikisha ushindani wa Ligi Kuu Z’bar unasimamiwa kwa haki, weledi na kwa kuzingatia sheria za mchezo.