Vita ya ufungaji ZPL, ukizubaa unaachwa
Muktasari:
- Mshambuliaji wa Zimamoto, Rashid Said, hivi sasa ndiye anayeongoza mbio hizo za ufungaji baada ya kufumania nyavu mara nne akifunga dhidi ya Wembe, KMKM, Muembe Makumbi na Mafunzo.
VITA ya ufungaji bora katika Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL) imeshika kasi huku wanne kati yao wakiwemo watatu washambuliaji na mmoja kiungo wakionesha kiu kubwa ya kuzifumania nyavu kila wanaposhuka dimbani.
Mshambuliaji wa Zimamoto, Rashid Said, hivi sasa ndiye anayeongoza mbio hizo za ufungaji baada ya kufumania nyavu mara nne akifunga dhidi ya Wembe, KMKM, Muembe Makumbi na Mafunzo.
Hata hivyo, Rashid ana kazi kubwa ya kufanya kwani anafuatiwa kwa ukaribu na nyota watatu wenye mabao matatu kila mmoja.
Mshambuliaji wa KVZ, Mohamed Mussa ‘Banega’ mabao yake matatu ameyafunga dhidi ya Fufuni na Raskazone akitupia mawili.
Ufundi wa Banega pamoja na utulivu wake anapokabiliana na makipa, umemweka pazuri katika mbio hizo za ufungaji bora.
Siyo Banega pekee anayemnyemelea Rashid, kwani Yahya Haji Salmin ‘Karoa’ wa Uhamiaji naye yumo katika vita hiyo akiwa na mabao matatu akifunga katika mechi dhidi ya Mwenge, Chipukizi na Fufuni.
Orodha hiyo ya wenye mabao matatu ni kiungo wa kati wa KVZ, Yakoub Said ‘Kane Ally’ ambaye alifunga dhidi ya Mlandege, Raskazone na JKU.
Katika vita hiyo, Yakoub ni kiungo pekee aliyeingia mapema kuwania ufungaji bora dhidi ya washambuliaji.
Ligi hiyo inapozidi kushika kasi, ni wazi kuwa vita ya ufungaji bora kwenye ZPL bado mbichi kabisa na yeyote anaweza kuibuka kidedea.
Ikumbukwe kuwa msimu uliopita kwenye ligi hiyo mfungaji bora alikuwa Michael Joseph akiwa KVZ aliyefunga mabao 21 akicheza mechi 29.