KMKM hali ni mbaya Ligi Kuu Zanzibar
Muktasari:
- KMKM iliyoishia hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kufungwa jumla ya mabao 7-0 dhidi ya Al Ahli Tripoli, pointi moja iliyoipata katika Ligi Kuu Zanzibar ilikuwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mafunzo, Septemba 20, 2026.
WALIOKUWA wawakilishi wa Zanzibar katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu 2026-2027, KMKM, hali yao ndani ya Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) ni mbaya baada ya kukusanya pointi moja kwenye mechi nne ilizocheza.
KMKM iliyoishia hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kufungwa jumla ya mabao 7-0 dhidi ya Al Ahli Tripoli, pointi moja iliyoipata katika Ligi Kuu Zanzibar ilikuwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mafunzo, Septemba 20, 2026.
Timu hiyo juzi ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Raskazone kwenye Uwanja wa Mao A, kisiwani Unguja. Kabla ya hapo, ilianza msimu kwa kufungwa 2-1 na Kipanga, kisha ikalala mbele ya Zimamoto kwa mabao 2-1. Mechi zote zikichezwa Unguja.
Matokeo hayo yanaifanya KMKM kukamata nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar kati ya timu 16, ikiwa imefunga mabao matatu na kuruhusu sita baada ya mechi nne.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa KMKM, wapinzani wao Raskazone walioibuka na ushindi, taratibu wameanza kurejea.
Kabla ya mechi hiyo, Raskazone ilifungwa na KVZ mabao 4-0, kisha Uhamiaji bao 1-0, matokeo ambayo yalililazimu benchi la ufundi na uongozi wa timu hiyo kukaa chini na kusuka mipango kabla mambo hayajawaharibikia zaidi.
Mipango yao ilizaa matunda katika mchezo dhidi ya KMKM kwani dakika ya 84, Hafidh Omary aliiandikia bao pekee timu hiyo lililodumu hadi kumalizika kwake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Msaidizi wa Raskazone, Abdulghani Gulamu amesema mchezo huo ulikuwa na ushindani kwa pande zote lakini wao wamefanikiwa kuibuka washindi.
“Tulikosa matokea mazuri kwenye mechi mbili zilizopita, hiyo ilisababishwa na ugumu wa mechi na wachezaji kutokuwa makini, lakini tulilifanyia kazi hilo, tukashinda,” amesema.
Amesema kwa sasa timu hiyo inahitaji kufanya vizuri kusalia Ligi Kuu Zanzibar ndio sababu ya kupambania matokeo mazuri kwenye duru ya kwanza ya ligi hiyo.
Raskazone iliyopanda daraja msimu huu, ushindi huo umewapandisha hadi nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar kabla ya mechi za jana ikifikisha pointi saba, ikishinda mechi mbili sawa na ilizopoteza, huku sare ikiwa moja. Imefunga mabao matatu na kuruhusu sita.