Vita imeanza, Simba yatia mkono usajili Yanga

Monday June 07 2021
usajilii

KAZI imeanza. Ndio, ile vita ya usajili kwa vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga imeanza baada ya mabosi wa Msimbazi kuamua kutia mkono wao kwenye dili la usajili wa Mkongoman.

Ipo hivi. Ukiwauliza mashabiki wa Yanga juu ya beki Djuma Shaaban, wenyewe watakujibu, ‘tunamsubiria atue’, lakini habari hii inaweza kuwa mbaya kwao baada ya watani wao Simba kushtukia kitu kisha wakarejea kwa nguvu kwa beki huyo wa kulia wa AS Vita ya DR Congo.

Simba ndio ilikuwa klabu ya kwanza kumfuata Djuma, ikiwa ni siku chache tu tangu alipowasumbua kwenye mchezo wao wa kwanza makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa mjini Kinshasa na Wekundu hao kuibuka na ushindi mwembamba, lakini muhimu ugenini wa bao 1-0.

Hata hivyo, baadaye Simba iliamua kuachana naye baada ya kusikia amevunjika akiwa na kikosi cha timu ya taifa ya DR Congo na kutoa mwanya kwa Yanga kuingia kwa kasi kumfukuzia beki huyo wa kupanda na kushuka mwenye mikrosi ya hatari uwanjani.

Mwanaspoti, linafahamu Yanga chini ya Makamu mwenyekiti wa kamati ya Usajili, Injinia Hersi Ally Said imeshafanya mazungumzo karibu kila kitu na nahodha huyo wa mabingwa hao wa DR Congo, AS Vita na imebakiza hatua chache tu za kumshusha Jangwani, hata hivyo taarifa za uhakika kutoka Simba, Msimbazi wanataka kupindua meza kibabe.

Inaelezwa bosi mmoja karibu kabisa na Mohamed Dewji ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Simba amepiga simu Kongo kisha kuambiwa kila kitu juu ya Yanga walikofikia.

Advertisement

Bosi huyo haraka haraka, akaomba siku tatu kutoka jana akiahidi kumalizana nao kwani wameamua kurudisha mawindo yao kwa beki huyo waliyekuwa wakimsubiria ampone majeraha yake.

Hatua hiyo inakuja kufuatia bosi huyo wa Simba kuambiwa bado Yanga hawajamaliza dili hilo na kigogo hyo amelifichulia Mwanaspoti kocha wao Didier Gomes amefungua milango ya usajili wa beki huyo.

Hesabu za Simba ni msimu huu beki wao wa kulia aliyecheza kwa zaidi ya asilimia 95 Shomari Kapombe, anaweza kuchoka endapo ataendelea kutumika katika kila mchezo, kwani msaidizi wake kwenye nafasi hiyo, kinda David Kameta ‘Duchu’ akishindwa kumpa ushindani wa namba mkongwe huyo.

“Gomes ameshaweka wazi anahitaji beki, ndio maana tumeamua kurudi tena kwa Djuma, kama dili litafanikiwa itakuwa bomba, ili nafasi ya Kapombe isitupe presha kubwa,” chanzo hicho kilisema.


MSIKIE DJUMA

Mara baada ya kupata taarifa hiyo, fasta Mwanaspoti liliamua kumvutia waya, beki huyo na kuongeza naye kutoka DR Congo.

Djuma aliliambia Mwanaspoti ni kweli amekuwa katika mazungumzo na Yanga kwa takribani zaidi ya wiki moja na nusu, japo bado hawajamalizana nao, lakini Simba nao wamerudi wakihitaji huduma yake.

“Ni kweli mabosi wa Simba nao wamerudi tena kwangu kupitia wakala na viongozi, huku pia tayari nikiwa imeshaanza mazungumzo na Yanga, bado nasikilizia,” alisema Djuma.

Beki huyo alipoulizwa anaweza kuibukia wapi kupitia dili hilo na kujibu kwake hakuna shida kucheza kokote, ilimradi timu itakayowahi kumalizana naye na klabu yake ya Vita iridhie basi atakuwa tayari kuichezea.

“Yanga sijamalizana nao, ingawa tumeshakubaliana karibu kila kitu, tuna muda sasa hatujafikia hatua ya kumaliza kila kitu ingawa najua wanaongea kwa karibu na meneja wangu,” alisema Djuma na kuongeza;

“Sasa naona Simba nao wamekuja tena wananiuliza kama nimeshasaini Yanga, nimewajibu bado ila tuko katika hatua nzuri nimewaambia (Simba) wamtafute meneja wangu waongee naye, mimi kazi yangu kucheza mpira hizo Simba na Yanga zote ni timu kubwa wako marafiki zangu wamecheza hapo, hivyo atakayemalizana na mimi nitakuja kucheza.”

Yanga ilionekana imepata urahisi wa kumnyakua beki huyo, baada ya Simba kumkaushia kutokana na sharti lake kwamba hataki kukalishwa benchi, wakati kwa sasa moto wa Kapombe ni vigumu kuzimwa kirahisi ndani ya kikosi hicho cha Msimbazi.

Ndani ya kikosi cha Yanga kwa sasa kina mabeki wawili wenye viwango sawa, Kibwana Shomary na Paul Godfrey ‘Boxer’ ambao wamekuwa wakipeana nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.

Advertisement