Vigogo Simba kukutana Dar kesho
Muktasari:
- Taarifa iliyotolewa leo Jumapili na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori, ilisema baada ya kikao hicho cha Bodi, tarehe ya kufanyika kwa mkutano mkuu itawekwa wazi.
KLABU ya Simba, imetangaza kuwa, kesho Jumatatu kutakuwa na kikao cha Bodi ya Wakurugenzi kujadili ajenda ya Mkutano Mkuu maalum wa Wanachama.
Taarifa iliyotolewa leo Jumapili na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori, ilisema baada ya kikao hicho cha Bodi, tarehe ya kufanyika kwa mkutano mkuu itawekwa wazi.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa taarifa zilizobainisha kuwa, Klabu ya Simba leo Jumapili ilifanya Mkutano Mkuu wa dharula na dua maeneo ya Bunju, Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, taarifa zilieleza limeundwa Baraza la Wadhamini Jipya la Simba SC ambapo waliopitishwa kuunda baraza hilo ni Salim Abdallah Muhene, Dk Bill Kiwia, Alhaj Ismail Mohamed, Amos Makala, Adam Mgoi, Hamad Abdallah na Hassan Hasanoo.
“Tunapenda kuwataarifu wanachama wote wa Simba kuwa hicho kilichofanyika Bunju siku ya leo siyo kikao rasmi cha mkutano maalum wa Simba. Hivyo maamuzi yote yaliyotangazwa huko ni batili na kinyume cha Katiba ya Simba,” ilisema taarifa hiyo.
“Kwa mujibu wa Katiba ya Simba ya mwaka 2018 iliyofanyiwa marekebisho 2026, ibara ya 23, Mkutano Mkuu maalum utaandaliwa na Mwenyekiti wa Klabu kwa kushirikiana na Bodi ya Wakurugenzi. Hivyo kesho (kesho) tarehe 3/8/2026 kutakuwa na kikao cha Bodi kujadili ajenda ya Mkutano Mkuu maalum wa Wanachama. Mtajulishwa siku maalum ya Mkutano huo.”