Mariam Yusuph ni mama, mke na mchezaji
Muktasari:
- Mwanaspoti limefanya mahojiano na Mariam, anazungumzia namna wachezaji wakiamua kutenganisha kazi na kusimamia misingi ya uhalisia wa mwanamke, watasaidia kuweka wepesi kwa wazazi kuwaruhusu mabinti kuonyesha vipaji vyao.
BEKI wa Mashujaa Queens, Mariam Yusuph Juma mwenye umri wa miaka 33, ameamua kuonyesha mfano kwa matendo, kutenganisha kazi anayoifanya ya soka na maisha halisi kama mwanamke.
Mwanaspoti limefanya mahojiano na Mariam, anazungumzia namna wachezaji wakiamua kutenganisha kazi na kusimamia misingi ya uhalisia wa mwanamke, watasaidia kuweka wepesi kwa wazazi kuwaruhusu mabinti kuonyesha vipaji vyao.
"Baadhi ya wazazi inakuwa ngumu kuwaruhusu watoto wao wa kike kucheza mpira, wakiamini miongoni mwao wanavaa kihuni, wanaona kama ni mlango wa watoto wao kuharibikiwa," anasema Mariam na kuongeza;
"Mfano mchezaji wa kike unakuwa amevaa suruali mlegezo nguo za ndani zinakuwa zinaonekana, anatembea kwa kudundika kama mwanamume, wakati mwingine anavyonyoa nywele hata kijana wa kiume anayezingatia maadili hawezi kunyoa hivyo.
"Hiyo inakuwa sababu ya wengi wao kushindwa kuanzisha familia, wakati mwingine inakuwa ngumu kwa mwanamume kumwona kama ni mwenza wa safari yake ya maisha, kwani wanakuwa hawaonyeshi kama wanaweza wakawa ni mama wa baadaye."
NDOA NA SOKA
Anasema ameolewa na ana watoto watatu na mume wake, lakini hilo halijawa kikwazo cha kufanya majukumu yake kama kawaida.
"Kwa mara ya kwanza nilikutana na mume wangu mwaka 2010, alikuwa ni mchezaji lakini kwa timu za madaraja ya chini, alikuwa anapenda uchezaji wangu, mwaka 2014 tulifunga ndoa kanisani, kipindi chote tangu nikutane naye amekuwa ananisapoti kazi zangu na kuhakikisha kipaji changu hakirudi nyuma," anasema Mariam na kuongeza;
"Mwanangu wa kwanza nilimzaa mwaka 2012 nikiwa katika kituo cha Marsh Queens, wakati mwanangu bado mdogo nilipata timu ya Kinondoni iliyokuwa inacheza Taifa Cup, mkataba niliyoingia nao niliwaambia lazima wazingatie kuhusu mtoto wangu, hivyo nikawa nakaa naye kambini na walinitafutia mtu wa kumhudumia nikiwa mazoezini au kwenye mechi.
"Mwaka 2015 nilisajiliwa na Mburahati Queens kipindi hicho mchezaji wa daraja la juu, tulikuwa tunapewa Sh100,000 na viatu, hakukuwa na mshahara zaidi ya posho, hivyo pesa ndogo ndogo nilikuwa nazitunza ili kufanya mahitaji muhimu.
"Nikiwa na Mburahati Queens nilipata ujauzito wa mtoto wangu wa pili, niliendelea kufanya mazoezi na timu hadi ilipofika miezi saba nikaona inatosha nikarudi nyumbani ili nijifungue, ingawa kipindi hicho hakukuwa na pesa, nakumbuka viongozi walikuwa na ushirikiano na mimi na waliheshimu hatua yangu ya kuwa na familia.
Anasema baada ya mtoto wake kufikisha umri wa mwaka mmoja, alisajiliwa na Kigoma Sisters kwa mkataba wa misimu miwili 2016/17 na 2017/18 na alizingatia kuweka vipenge vya watoto wake.
"Nilisaini mikataba mitatu ya mtoto wangu ambaye nilimuacha nyumbani na mama yangu, alikuwa anatumiwa Sh.200,000 kila mwezi, mwingine ulikuwa wa mtoto wangu wa mwaka mmoja ambaye nilienda naye kambini, huyo alikuwa anasimamiwa matibabu, chakula na walinitafutia mtu wa kumhudumia muda ambao nilikuwa mazoezini na kwenye mechi pamoja na mkataba wangu mwenyewe," anasema.
Anasema baada ya kumaliza mkataba na timu hiyo, alirejea kuichezea Marsh Queens, lakini mwaka 2020 alipata mimba tena: "Mimi ni mke wa mtu, nikirudi nyumbani likizo, nakutana na mume wangu kimwili, nikajikuta napata mimba ya mtoto wangu wa tatu, ambayo nikawa naumwaumwa, ilipofika miezi mitatu ilibidi niwaambie viongozi na walinielewa, hivyo ilibidi niende kwa mama yangu Mwanza ili nipate usimamizi na usaidizi.
Anaongeza: "Baada ya kujifungua nilipofikisha miezi mitatu, viongozi wa timu ya Tiger Queens walinifuata ili wanisajili, nikawaambia ukweli nina mtoto ana miezi mitatu, kama watanichukua nitaingia mkataba wa mimi na mwanangu, walikubari nikaenda na mwanangu kambini nikatafutiwa dada wa kumtunza.
"Baada ya kuichezea timu hiyo niliitwa timu ya taifa ya Twiga Stars mwaka 2021 kwenda kucheza michuano ya Kombe la Cecafa, tulichukua ubingwa huo ilikuwa ni Afrika Kusini, baada ya kurejea nyumbani Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu alitupatia viwanja Dodoma."
KUTUNZA MWILI
Anasema kuna vitu anavizingatia akitoka kujifungua, vinavyomsaidia kurejesha nguvu ya kupambana na kucheza hadi sasa.
"Wiki la kwanza nikitoka kujifungua, nakuwa na zoezi la kutembea kwa mita kadha kila siku, wiki la pili nakuwa nafanya mazoezi ya kukimbia, wiki la tatu naanza kuchezea mipira uwanjani na wiki la nne, nakuwa nimelikavaa na kupata nguvu ya kuanza kufanya mazoezini na wenzangu," anasema na kuongeza:
"Jambo lingine ninalolifanya, naepukana kabisa na vyakula vya mafuta, soda ambazo mara nyingi zinasababisha gesi, badala yake nakunywa maji kwa wingi pamoja na kutumia matunda, hivyo vinanifanya niutunze mwili wangu kuendelea kukaa vizuri."
UWANJANI, AMTAJA YONDANI
Anasema ukiondoa kuwa kipa pia ni kiraka anayecheza namba zote uwanjani, hivyo timu alizozichezea ikitokea mchezaji akikosekana alikuwa anaziba pengo na haikuwahi kuwa kitu kigumu kwake.
"Kwa sasa nacheza beki ya kati, tofauti na mwanzo ambako nilikuwa nacheza nafasi zote uwanjani, waliyonishuhudia wakati nacheza hao ndiyo wanajua uwezo wangu," anasema Mariam anayemtaja staa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Kelvin Yondani kuwa alikuwa aikoni kwake.
MASHUJAA IMEMPA PESA NDEFU
Anasema kwa mara ya kwanza timu iliyompa dau kubwa la usajili Sh.5 Milioni ni Mashujaa, jambo ambalo limezidi kumuongezea chachu ya kujituma zaidi.
"Uongozi wa Mashujaa umenyooka sana, nakumbuka baada ya kukubaliana nisaini miaka miwili, walinipa pesa yangu yote, viongozi wanajali zaidi maisha ya wachezaji, nafurahia kuwa sehemu ya kikosi chao," anasema Mariam na kuongeza;
"Kuna timu unaweza ukakubaliana nao, dau la Sh.10 Milioni lakini hawakupi, tofauti na hapa nimepewa na nimefanya jambo la msingi zaidi."
Ukiondoa Mashujaa anaitaja timu ya Tausi FC kwamba ndiyo ilikuwa inamlipa mshahara mkubwa wa Sh.700,000:
"Mashujaa iliniona nikiwa na timu ya Tausi, baada ya kucheza mechi dhidi ya Yanga Princess na Foutain Gate, nilipoona ofa yao imenyoka nikakubali kufanya nayo kazi kuanzia msimu huu."
JASHO LAKE LA SOKA
Anasema kabla ya baba yake mzazi kufariki mwaka 2018, alikuwa anamsapoti katika mazoezi na kumsisitiza anamtegemea aje kumtunza mama yake.
"Maneno ya baba yangu yanaishi kwa matendo, nimemjengea nyumba Mwanza kwa sasa anakaa kwenye mji wake, naendelea kumtunza yeye na bibi, kwetu tumezaliwa 12 mimi ni mtoto wa pili kutoka mwisho na tuliyopo duniani ni sita.
"Pia naendelea na ujenzi wa nyumba yangu, Mungu akipenda hadi mwakani huenda ikakamilika, nimefanya hayo yote kupitia jasho la soka, ndiyo maana nacheza kwa nidhamu ya hali ya juu, isingekuwa hivyo huenda nisingekuwa hapa nilipo leo."
Kitu kingine alichokifanya ameanzisha kitu cha soka mwaka 2022, kinachoitwa Mamu Sports Center kilichopo Kitunda Mwanagati, kina jumla ya wachezaji 58, kina wasichana 20 na wavulana 18.
"Kina watoto wa kuanzia miaka 10 hadi 13 na 15 hadi 17, anayekisimamia ni mume wangu Josephart Mikao na kati ya mambo ninayowasisitiza wasichana ni kulinda asili yao na kujua ni mama wa baadaye, natamani kiwe kituo chenye mfano wa kuitwa," anasema Mariam na kuongeza;
"Naomba wadhamini ambao wanaweza wakaniunga mkono harakati zangu, naamini wakinisaidia wanakuwa wamesaidia ndoto za wasichana na wavulana wengi ambao watakuja kulipwa na vipaji vyao.'
Anasema nguvu kubwa ya kufanya hayo yote anaipata kutoka kwa watoto, mume na wazazi wake ambao ndio mashabiki wake namba moja: "Mfano kama tulikuwa na mechi, nikirudi nyumbani wanangu wananiambia mama pale ulikosea kupiga ulitakiwa ufanye hivi, inanipa moyo sana, mume wangu huwa anakuja na watoto uwanjani kuja kuona kile ninachokifanya na nawasomesha kupitia mpira wa miguu."
Anasema japokuwa mume wake hana wazazi, lakini yupo dada yao mkubwa anayemchukulia kama mama yake mkwe.
"Kuna siku tuliruhusiwa tukapumzike na familia zetu, nikaambiwa wifi ambaye namchukulia kama mama mkwe anahitaji nikamuone, ilinibidi niende nyumbani nikavae mavazi ya staha, ndipo nikaenda kumuona, ni watu ambao wananisapoti pia."