Muhubu aipa JKT Queens tiketi fainali ya Ngao ya Jamii
Muktasari:
- Shujaa wa JKT Queens katika mchezo huo alikuwa Fatuma Muhubu aliyefunga bao pekee dakika ya 48, lililoiwezesha timu hiyo kupata ushindi muhimu na kukata tiketi ya kucheza fainali ya michuano hiyo itakayopigwa Oktoba 3, 2026.
JKT QUEENS imefanikiwa kutinga fainali ya Ngao ya Jamii kwa wanawake baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa Queens katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza uliopigwa leo Septemba 30, 2026 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Shujaa wa JKT Queens katika mchezo huo alikuwa Fatuma Muhubu aliyefunga bao pekee dakika ya 48, lililoiwezesha timu hiyo kupata ushindi muhimu na kukata tiketi ya kucheza fainali ya michuano hiyo itakayopigwa Oktoba 3, 2026.
JKT Queens ambayo ilimaliza Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) msimu uliopita ikiwa nafasi ya pili, imeonyesha dhamira ya kuanza msimu mpya kwa mafanikio kwa kutumia nafasi muhimu iliyopatikana kipindi cha pili.
Bao la Muhubu limekuja katika mchezo ambao ulikuwa muhimu wa kutafuta nafasi ya kutetea taji hilo ililobeba mara mbili mfululizo mwaka 2024 na 2025.
Kwa ushindi huo, JKT Queens sasa itasubiri mshindi wa nusu fainali ya pili unayozikutanisha Simba Queens na Yanga Princess.
Mchezo wa Simba Queens na Yanga Princess unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na historia ya timu hizo kukutana katika mechi zenye presha.