Simba Queens yaichapa tena Yanga Princess ikifuzu fainali Ngao ya Jamii
Muktasari:
- Mchezo huo ulianza kwa ushindani mkali huku Simba ikitengeneza nafasi kadhaa za kulisogelea lango la Yanga, kabla ya Vivian Corazone kuifungia bao la kwanza dakika ya 23 na kuipa timu hiyo uongozi wa 1-0 kwenye kipindi cha kwanza.
SIMBA QUEENS imefuzu kucheza fainali ya Ngao ya Jamii kwa Wanawake baada ya kuichapa Yanga Princess mabao 3-0 katika nusu fainali ya pili iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, na sasa itakutana na JKT Queens Oktoba 3, 2026 kwenye fainali.
Mchezo huo ulianza kwa ushindani mkali huku Simba ikitengeneza nafasi kadhaa za kulisogelea lango la Yanga, kabla ya Vivian Corazone kuifungia bao la kwanza dakika ya 23 na kuipa timu hiyo uongozi wa 1-0 kwenye kipindi cha kwanza.
Yanga ilipata pigo dakika ya 36 baada ya Ritticia Nabbosa kuonyeshwa kadi nyekundu kufuatia kumchezea madhambi Mary Siyame wa Simba, hali iliyowafanya Wananchi kucheza pungufu kwa sehemu kubwa iliyosalia ya mchezo.
Ikiwa na faida ya mchezaji mmoja zaidi, Simba iliendelea kulisakama lango la Yanga na juhudi zake zilizaa matunda dakika ya 57, Senaf Demise akafunga bao la pili kabla ya Mary Siyame kufunga la tatu dakika ya 90 na kuifanya Simba Queens kupata ushindi wa mabao 3-0.
Matokeo hayo yanaifanya Simba Queens kutinga fainali na sasa itakutana na JKT Queens ambayo ilipata tiketi hiyo baada ya kuifunga Mashujaa Queens bao 1-0, bao pekee likifungwa na Fatuma Muhubu dakika ya 48.
Fainali hiyo itakayopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex itakuwa marudiano ya fainali ya mwaka jana, ambayo JKT Queens iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba Queens na kutwaa Ngao ya Jamii kwa mara ya pili mfululizo.
Hata hivyo, historia ya timu hizi kwenye mashindano hayo inaonyesha zimekutana katika fainali mbili, mwaka 2023 Simba Queens ikitwaa taji baada ya sare ya 1-1 na kushinda kwa penalti, kabla ya JKT Queens kulipa kisasi mwaka 2025 kwa ushindi wa 2-1. Hivyo Simba itakuwa na nafasi ya kutafuta kulipa kisasi, huku JKT ikisaka kuendeleza ubabe wake mbele ya Wekundu hao wa Msimbazi.