Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Usajili 10 bora Ulaya wenye thamani ndogo msimu huu

MARSEILLE, UFARANSA: KUTOKA kwa washambuliaji wenye uzoefu hadi vipaji vyenye umri mdogo vinavyosisimua, hawa hapa ni wachezaji 10 ambao wanaweza kuthibitisha kuwa usajili wa bei nafuu kwa timu zao mpya msimu huu huko Ulaya.


Rodrigo Mora (Porto - Roma Pauni 21.4 milioni)

Hata katika zama hizi za kupanda bila kukoma kwa gharama za usajili, ada ya zaidi ya Pauni 20 milioni kwa kawaida haiwakilishi usajili wa bei nafuu.

Hata hivyo, uamuzi wa Roma kumsajili kiungo mshambuliaji wa Porto, Mora, unaweza kuwa tofauti, kwani mchezaji huyo alikuwa kwenye rada za timu kubwa za Ulaya tangu alipong’ara akiwa na Porto B akiwa na umri wa miaka 15, na Porto walikuwa tayari na kifungu chake cha kuachiwa cha Pauni 59.5 milioni msimu uliopita 2025. Hilo halikutokea na Mora baadaye akaanza kupoteza nafasi chini ya kocha mpya, Francesco Farioli, kisha Roma ikatua na ofa ya Pauni 21.4 milioni pamoja na asilimia 50 ya ada ya mauzo yake ya baadaye ambayo inaweza kununuliwa.

Uhamisho huo pia ulimvutia Mora, ambaye alikuwa na hamu ya kufanya kazi chini ya Gian Piero Gasperini. “Alikuwa na nafasi kubwa katika uamuzi wangu wa kuja hapa kwa sababu anapenda wachezaji wenye sifa kama zangu, na mimi ni shabiki wa namna anavyotaka timu zake zicheze,” Mora alisema.

Dalili za awali ni nzuri, huku Mora akifunga bao lake la kwanza la Roma dhidi ya Lecce, wakati Giallorossi walipoanza kwa kasi msimu wao wa Serie A.


Elliot Stroud (Mjallby- Hull Pauni 3.5 milioni)

Kupanda Ligi Kuu England ni jambo linalogharimu fedha nyingi, lakini Ipswich, Coventry na Hull kwa pamoja zilitumia Pauni 450 milioni zaidi ya mapato yao katika usajili wa wachezaji msimu huu. Katika uwekezaji huo mkubwa, uamuzi wa Hull kumsajili Stroud, mwenye umri wa miaka 24, raia wa Sweden unaonekana kuwa biashara nzuri.

Mchezaji huyo wa pembeni alikuwa mmoja wa waliong’ara zaidi kwa Mjallby wakati timu hiyo  ya mji mdogo ilipotwaa ubingwa wa Sweden mwaka jana, jambo lililompa nafasi katika kikosi cha Graham Potter cha Kombe la Dunia.

Kocha wa Hully City, Sergej Jakirovic alimtambua kama nyongeza muhimu katika kikosi baada ya kushinda mechi ya mchujo wa kupanda daraja.

“Ni mchezaji mzuri sana; anaweza kucheza nafasi nyingi. Anaweza kucheza beki wa pembeni, wing-back, winga wa kushoto na katikati. Pia ni mchezaji anayekimbia sana, hivyo nadhani atatufaa sana,” alisema kocha huyo. Stroud amekuwa chaguo la haraka na lenye ubunifu kwa kikosi cha Jakirovic kinachopambana sana uwanjani ili kupata matokeo.


Aubameyang (Marseille - Deportivo Pauni 1.3 milioni)

Kwa mtazamo wa kwanza, kulipa kiasi kidogo cha fedha kumsajili mshambuliaji mwenye kiwango na uzoefu wa Pierre-Emerick Aubameyang ni uamuzi usiohitaji kufikiriwa sana.

Hata hivyo, mchezaji huyo wa zamani wa Arsenal na Borussia Dortmund ana miaka 37 na amekuwa na safari ya kuhamahama tangu alipoondoka Barcelona. Kipindi kisichokuwa na mafanikio Chelsea kilifuatiwa na misimu miwili Marseille, huku katikati kukiwa na mwaka mmoja Al-Qadsiah nchini Saudi Arabia.

Lakini, kiwango chake cha kufunga mabao kimekuwa cha kuvutia akifunga mabao 44 katika misimu mitatu iliyopita, na imeripotiwa kuwa amekubali mshahara uliopunguzwa kwa kiasi kikubwa ili acheze mara kwa mara La Liga. Mradi wa Deportivo wenye malengo makubwa unaonekana kumfaa kikamilifu, huku akiwa amefunga mabao matano katika mechi saba za ligi.


USAJI 04

Satoshi Tanaka (Fortuna - Schalke Pauni 900,000)

Timu tatu zilizopanda Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga), tofauti kubwa na za England zilitumia kwa pamoja Pauni 7.2 milioni zaidi ya mapato yao katika usajili msimu huu. Mabingwa wa Bundesliga 2 (Daraja la Pili), Schalke walifanikiwa kusajili kwa mkopo baadhi ya majina yanayojulikana akiwemo shabiki wao wa tangu utotoni Robin Gosens, lakini kiungo mkabaji Tanaka ndiye mchezaji wa kudumu aliyewgharimu zaidi, Pauni 900,000.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 bado ni kamari kwa kiasi fulani, kwani uzoefu wake pekee wa awali wa soka la Ujerumani ulikuwa tangu Januari akiwa na Fortuna Dusseldorf, ambayo ilishushwa daraja hadi Ligi ya Daraja la Tatu.

Hata hivyo, Tanaka alimvutia mkurugenzi wa soka wa Schalke, Youri Mulder, aliyesema: “Bidii yake na nguvu zake vinaendana vizuri sana na aina yetu ya mchezo.”

Katika mechi yake ya kwanza ya Bundesliga, uwezo wa Tanaka wa kupambana uliisaidia timu yake kuilazimisha Bayern Munich sare ya bila kufungana, na anaweza kuwa muhimu katika kuamua kama Schalke itaepuka matatizo msimu huu.


USAJI 05

Nico Elvedi (Gladbach - Leeds Pauni 6.8 milioni)

Leeds United wana mfumo wao ulio wazi wa usajili; kusajili wachezaji wanaotegemewa, wenye uzoefu na sifa nzuri za kimwili, ikiwezekana kutoka Bundesliga. Beki wa kati wa Uswisi, Nico Elvedi anaendana kikamilifu na mfumo. Kocha wa timu hiyo, Daniel Farke huenda alitarajia kipindi cha kuzoea kwa mchezaji ambaye alikuwa ametumia miaka 11 Borussia Monchengladbach.

Badala yake, Elvedi amezoea haraka akiwa pamoja na mchezaji mpya mwenzake Tarik Muharemovic, akicheza zaidi upande wa kushoto wa mabeki watatu. Ni muungano wa kufurahisha kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 na kocha wake wa zamani wa Gladbach.

“Ulikuwa mwaka mmoja tu (alipokuwa kocha Gladbach, lakini nilimpenda kama kocha. Nilijifunza mengi kutoka kwake na sasa nitajifunza mengi zaidi,” Elvedi alisema kumhusu Farke na tayari anajifunza kwa kasi.


USAJI 06

Gabriel Vidovic (Dinamo - Paderborn Pauni 2.6 milioni)

Paderborn wamerejea Bundesliga kwa kishindo baada ya kuishtua Wolfsburg katika mchujo wa kupanda/kushuka daraja, huku wakivunja rekodi ya usajili ambayo ilikuwa Pauni 700,000 kwa kumsajili Gabriel Vidovic na mshambuliaji Marvin Pieringer kwa Pauni 2.6 milioni kila mmoja.

Vidovic ni zao la akademi ya zamani ya Bayern Munich na kurejea kwake katika Ligi Kuu Ujerumani ni jambo la kuvutia.

Alilelewa Bayern chini ya Julian Nagelsmann, lakini kiungo huyo mshambuliaji wa Croatia alishindwa kuwa mchezaji wa kudumu katika kikosi hicho. Kipindi kizuri cha mkopo Dinamo Zagreb kilimpa nafasi nyingine ya kuonyesha uwezo wake akiwa Mainz, lakini Vidovic alicheza mara chache sana na Bayern wakasitisha mkopo huo kabla ya muda wake.

Baada ya kurejea Dinamo kwa mkataba wa kudumu, uwezekano wa kucheza Bundesliga ulionekana kuwa mbali hadi Paderborn walipojitokeza.

“Wasifu wake wa kisoka unajieleza wenyewe,” alisema mkurugenzi wao wa soka, Sebastian Lange. Kuwasili kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 ni hatari kwa klabu yenye uwezo mdogo wa kifedha, lakini kiwango cha juu cha uwezo wake kilichoonekana kwa Nagelsmann kinafanya awe balaa.


USAJI 07

Giovanni Reyna (Gladbach - Strasbourg Pauni 2.6 milioni)

Ligue 1, ambayo hujitambulisha kama “ligi ya vipaji” huwaendeleza wachezaji vijana ambao baadaye huuzwa kwa ada kubwa.

Strasbourg, ambayo ni klabu mshirika wa Chelsea imejikita kwa karibu katika mfumo huo; wanne kati ya wachezaji waliowasajili msimu huu walitoka kwenye kundi kubwa la wachezaji wa akiba waliopo Cobham, huku Valentin Barco na Emmanuel Emegha wakihamia upande mwingine.

Reyna, licha ya kuwa na umri wa miaka 23, anaonekana kuwa mchezaji wa aina tofauti.

Mchezaji huyo aliwahi kuwa dogo mwenye sifa kubwa na kufanya vizuri pamoja na Jude Bellingham na Erling Haaland katika kikosi cha Borussia Dortmund, lakini majeraha na kutokuwa na mwendelezo vikamkwamisha. 

Reyna alifungua mechi nne pekee za ligi katika msimu wake mmoja akiwa Gladbach, lakini ameanza vizuri nchini Ufaransa. Alifunga bao lake la kwanza kwa Strasbourg katika ushindi wa 6-2 dhidi ya Troyes mapema Septemba; iwapo ataendelea kuwa fiti na kutumia vyema mwanzo huu mpya, huenda isiwe muda mrefu kabla ya kuhusishwa na uhamisho wa kuvuka mpaka.


USAJI 08

Flavio Nazinho (Brugge - Monaco Pauni 4.3 milioni)

Beki wa kushoto mwenye uwezo wa kushambulia ambaye aliwahi kutajwa kuwa mrithi wa Nuno Mendes, Nazinho aliitwa katika kikosi cha kwanza cha Sporting na kocha wa zamani Ruben Amorim, lakini alicheza mechi 11 pekee kabla ya kurejea katika timu ya akiba.

Awali alipelekwa kwa mkopo Cercle Brugge 2023, kabla ya uhamisho huo kuwa wa kudumu dirisha lililofuata, na kupata muda wa kutosha wa kucheza kulianza kuzaa matokeo.

Baada ya kufunga mabao manne na kutoa asisti nane msimu uliopita, Nazinho alichukuliwa na klabu mshirika wa Cercle, Monaco. Ameanza kuleta athari mara moja akianzisha ushirikiano wa upande wa kushoto pamoja na Stanis Idumbo wakati kikosi hicho cha  kocha Filipe Luis kikiwa kileleni mwa Ligue 1. Kucheza Conference League kutampa Nazinho fursa zaidi kuamini uwezo wake wa kushambulia, na huenda akapata nafasi ya kwanza kuitwa katika timu ya taifa ya Ureno.


USAJI 09

Fran Garcia (Madrid - Betis Pauni 3.2 milioni)

Real Betis waliwahi kuzizidi klabu kadhaa za Ligi kuu England kumsajili mshambuliaji mwenye mabao mengi, Troy Parrott, ambaye haraka alionyesha thamani yake kwa kufunga bao la ushindi dhidi ya Real Madrid. Raia huyo wa Ireland aliigharimu Betis Pauni 17 milioni, ingawa ada hiyo bila shaka ingekuwa kubwa zaidi kama Parrott angekuwa anarudi Spurs badala ya kwenda Sevilla.

García, beki wa kushoto, huenda ndiye usajili wa bei rahisi zaidi wa msimu huu akiuzwa kwa Pauni 3.2 milioni pamoja na asilimia 50 ya ada yoyote ya mauzo yake ya baadaye wakati Madrid ilipokuwa ikipunguza kundi la wachezaji wake wasio muhimu.

Na akiwa na umri wa miaka 27, anaelekea kwenye kilele cha uwezo wake na ana uzoefu mkubwa wa mechi kubwa, akiwa ameichezea Madrid zaidi ya mara 100 na misimu miwili kamili kwa mkopo Rayo Vallecano. Garcia aliwahi kuhusishwa na Fulham dirisha lililopita; kocha Alvaro Arbeloa huenda akajutia kuiachia Betis kumsajili.


USAJI 10

Ainsley (Lyon - Everton Pauni 4.3 milioni)

Everton walipitia siku ya mwisho ya dirisha la usajili yenye msukosuko mkubwa, hali iliyomwacha kocha David Moyes akiwa na mshambuliaji mmoja tu wa kikosi cha kwanza na kikosi kipana. Angalau walifanikiwa kukamilisha kwa kuchelewa usajili wa Ainsley Maitland-Niles, mchezaji mwenye uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali aliyepatikana kwa bei nzuri.

Kuwasili kwa beki huyo wa zamani wa Arsenal huenda hakukutuliza mashabiki waliokuwa wamekasirika, lakini bao lake la kusawazisha dhidi ya Manchester United majuzi huenda tayari limerudisha sehemu kubwa ya thamani ya fedha zilizotumika kumsajili.