Uzoefu wampagawisha mido Rhino Rangers
Muktasari:
Nyota huyo wa zamani wa Biashara United, amejiunga na timu hiyo msimu huu wa 2026-2027, baada ya kuachana na Malindi FC inayocheza Ligi Kuu ya Zanzibar, aliyojiunga nayo dirisha dogo la Januari 2026, akitokea Stand United 'Chama la 'Wana'.
KIUNGO mshambuliaji wa Rhino Rangers ya Tabora Mjini, Pascas Wagana amesema uzoefu alionao anaamini utakuwa chachu ya kukisaidia kikosi hicho kuongeza ushindani msimu huu wa 2026-2027, licha ya ugumu mkubwa uliopo wa Ligi ya Championship.
Akizungumza na Mwanaspoti, Wagana amesema baada ya kutokuwa na msimu mzuri wa 2025-2026, kutokana na majeraha ya mara kwa mara, ila kwa sasa yupo fiti kukipambania kikosi hicho, huku akiwaomba mashabiki wa Tabora kuendelea kuwapa sapoti.
"Nawaomba mashabiki zetu waendelee kutupa sapoti kwa sababu wao ni mchezaji wa 12, uwanjani, mwenendo wetu hadi sasa sio mbaya wala mzuri sana, ila unatupa mwanga wa kuendelea kupambana ili kupigania malengo tuliyojiwekea," amesema Wagana.
Wagana aliyekifungia kikosi hicho bao moja msimu huu, amesema umoja ndio siri itakayowapa tiketi ya kurudi Ligi Kuu Bara baada ya kusota kwa muda mrefu, tangu waliposhuka msimu wa 2013-2014, walipomaliza mkiani mwa nafasi ya 14 na pointi 16.