Ni wikiendi ya vita ya kileleni Championship
Muktasari:
- Katika mechi zilizochezwa jana, tulishuhudia Bandari Tanzania ikiikaribisha Stand United ‘Chama la Wana’, kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, huku pia Gunners FC ikicheza dhidi ya Bigman FC, kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.
LIGI ya Championship imeingia raundi ya sita jana Ijumaa kwa mechi tatu kuchezwa kwenye viwanja mbalimbali na nyingine zikiendelea leo Jumamosi na kesho Jumapili, huku vita kali kwa sasa ikiwa ni kuwania nafasi za juu hasa ile ya kwanza.
Katika mechi zilizochezwa jana, tulishuhudia Bandari Tanzania ikiikaribisha Stand United ‘Chama la Wana’, kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, huku pia Gunners FC ikicheza dhidi ya Bigman FC, kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.
Mechi nyingine iliyopigwa jana ilikuwa ni TMA FC, ambayo haijaonja ladha yoyote ya ushindi hadi sasa, ikicheza dhidi ya Songea United inayotafuta pia kushinda kwa mara ya kwanza, baada ya kutoka sare tatu na kupoteza mbili kati ya mitano.
Leo Jumamosi zitapigwa mechi tatu, huku inayosubiriwa zaidi kwa hamu ni ya maafande wa Transit Camp dhidi ya KMC FC, itakayopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni ya vita kali ya kushindania kileleni kwa timu hizo.
Transit Camp ndio timu inayoongoza kwa sasa ikiwa na pointi 13, baada ya kushinda mechi nne na kutoka sare moja, huku KMC FC ikishika nafasi ya pili na pointi zake 11, baada ya kushinda tatu na kutoka sare mbili kati ya tano iliyocheza.
Ugumu wa mechi hiyo unatokana na kiwango cha timu hizo hadi sasa, jambo linaloongeza mvuto wa kuisubiria kwa hamu kujua nini kitatokea, huku moja ya silaha kubwa kwa kikosi cha KMC FC ni kutokana na safu yake bora ya ushambuliaji iliyonayo.
Katika mechi tano ilizocheza kila timu hadi sasa, safu ya ushambuliaji ya Transit Camp imefunga mabao tisa na kuruhusu matatu, huku kwa upande wa wapinzani wao KMC FC, ikiwa imeshafunga mabao 13 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne.
Moja ya jambo la kuvutia, ni kutokana na washambuliaji wa timu zote na anayeongoza kwa ufungaji ni Hamdan Farhan wa Transit Camp na Ramadhan Hashim Kalanje wa KMC FC, ambao kila mmoja amefunga mabao matano na kukoleza vita hiyo zaidi.
Kocha Mkuu wa Transit Camp, Said Lyakuka alisema licha ya ugumu wa mechi hiyo ila wamejipanga kukabiliana na wapinzani wao, hususani kujiandaa vizuri kuhakikisha hawawapi nafasi kutokana na ubora mkubwa wa washambuliaji walionao KMC FC.
“Timu zote mbili zimekuwa na mwenendo mzuri na hata tofauti ya pointi kati yetu na wao ni mbili, hii inaonyesha itakuwa ni mechi nzuri na ya kuvutia, ingawa, malengo yetu benchi la ufundi ni kubaki nyumbani na pointi tatu,” alisema Lyakuka.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa KMC, Mohamed Muya alisema ugumu wa mechi hiyo unatokana na viwango bora vya timu hizo hadi sasa, ingawa jambo kubwa alilowasihi wachezaji wa kikosi hicho ni kuongeza umakini na kutumia vyema nafasi za kufunga.
Mechi nyingine ya leo, itapigwa kwenye Uwanja wa Halmashauri ya Chunya jijini, Mbeya na wenyeji KenGold iliyotoka kuchapwa kwa mabao 2-0, dhidi ya Transit Camp, itaikaribisha Mbeya Kwanza iliyolazimishwa sare ya mabao 2-2 na Mbuni FC.
Katika mechi tano ilizozicheza, timu zote zina pointi nne ila zimetofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa baada ya kushinda moja, sare moja na kutoa sare tatu na KenGold inashika nafasi ya 11, huku Mbeya Kwanza ikiwa nafasi ya 10.
Mechi ya mwisho leo Jumamosi, itapigwa kwenye Uwanja wa Sheikh, Amri, Abeid, jijini Arusha na Mbuni FC iliyotoka sare ya mabao 2-2, dhidi ya Mbeya Kwanza, itaikaribisha timu ya Kigamboni United, iliyoichapa Songea United mabao 2-0.
Katika mechi tano ilizocheza Mbuni FC imeshinda moja, sare moja na kupoteza tatu, ikiwa nafasi ya 12 na pointi nne, huku kwa upande wa Kigamboni United ikishinda tatu, ikitoka sare moja na kuchapwa moja, ikishika nafasi ya nne na pointi 10.
Raundi ya sita itahitimishwa kesho Jumapili kwa mechi mbili kuchezwa, ambapo kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Morogoro, wenyeji Mtibwa Sugar itakuwa na kibarua kigumu cha kupambana dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons kutoka jijini Mbeya.
Timu hizo zinakutana kwa mara ya kwanza tangu ziliposhuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara hadi Championship msimu wa 2025-2026, baada ya kutokuwa na mwenendo wa kuridhisha, jambo linaloongeza ushindani zaidi wa kupambania nafasi ya kurejea.
Mtibwa Sugar iliyoshinda mechi mbili, sare mbili na kupoteza moja kati ya tano, ikiwa nafasi ya nane na pointi nane pia, inakutana na Prisons, huku ikiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na IAA SC ya jijini, Arusha.
Kwa upande wa Prisons inayoshika nafasi ya tatu na pointi 10, baada ya kushinda mechi tatu, ikitoa sare moja na kupoteza moja, inakutana na Mtibwa Sugar ikiwa na kumbukumbu ya kutoa pia sare ya bao 1-1, dhidi ya Stand United ‘Chama la Wana’.
Kwenye Uwanja wa Sheikh, Amri, Abeid, jijini Arusha, IAA SC iliyotoka sare ya kufungana mabao 2-2, dhidi ya kikosi cha Mtibwa Sugar, itaikaribisha Rhino Rangers kutoka Tabora, yenye kumbukumbu nzuri ya kuifunga Bigman FC ya Tanga mabao 2-0.
IAA SC inayoshiriki Ligi ya Championship kwa mara ya kwanza msimu wa 2026-2027, katika mechi tano ilizocheza imeshinda moja, sare mbili na kupoteza mbili, ikiwa nafasi ya tisa na pointi tano, huku ikifunga mabao matano na kuruhusu manane.
Kwa upande wa Rhino Rangers iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu Bara msimu wa 2013-2014, ilipomaliza mkiani mwa nafasi ya 14 na pointi 16, katika mechi tano, imeshinda tatu, sare moja na kupoteza pia moja, ikiwa nafasi ya sita na pointi 10.