Utata waibuka Kombe la Mwenge Kagera
Muktasari:
- Kwa mujibu wa AYE Football Academy, sakata hilo lilianza katika hatua ya nusu fainali baada ya Wolves ya Mtukula kukutana na Greenland. Mchezo huo uliisha kwa dakika 90 na kwenda kwenye mikwaju ya penalti, lakini giza lilipoingia uamuzi ukafanywa mchezo huo urudiwe siku nyingine.
MASHINDANO ya Kombe la Mwenge yanayoendelea mkoani Kagera yameingia katika sintofahamu baada ya uongozi wa AYE Football Academy kulalamikia kile walichodai kuwa ni ukiukwaji wa kanuni, upendeleo na maamuzi yenye utata yaliyowakosesha nafasi ya kutwaa ubingwa michuano hiyo.
Kwa mujibu wa AYE Football Academy, sakata hilo lilianza katika hatua ya nusu fainali baada ya Wolves ya Mtukula kukutana na Greenland. Mchezo huo uliisha kwa dakika 90 na kwenda kwenye mikwaju ya penalti, lakini giza lilipoingia uamuzi ukafanywa mchezo huo urudiwe siku nyingine.
AYE Football Academy inadai kuwa mchezo huo ulipangwa kuchezwa tena baada ya siku mbili, lakini siku ya mchezo Wolves ilifika uwanjani kwa wakati huku Greenland ikichelewa kufika.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, waamuzi waliamua kuipa Wolves ushindi kwa pointi tatu kwa kuzingatia kanuni walizokuwa wakitumia.
Hata hivyo, AYE Football Academy inadai kuwa baada ya uamuzi huo kufanywa na waamuzi, viongozi wa kamati ya maandalizi na baadhi ya viongozi wa michezo waliingilia suala hilo na kuamua mchezo urudiwe tena, jambo ambalo limeibua maswali kuhusu mamlaka ya kubadilisha uamuzi wa waamuzi ndani ya mashindano.
Kwa mujibu wa malalamiko hayo, Wolves ilipinga uamuzi huo na haikwenda kucheza mchezo uliopangwa upya, hali iliyosababisha Greenland kupewa nafasi ya kwenda moja kwa moja kwenye fainali ambako ilikutana na AYE Football Academy.
Sakata jingine lililolalamikiwa ni matumizi ya mchezaji wa Greenland anayefahamika kwa jina la Gatuso, mwenye jezi namba 11, ambaye AYE Football Academy inadai alipata kadi nyekundu katika mchezo wao wa awali lakini akashiriki tena katika fainali.
“Tumemwambia kamishna kuhusu hilo, lakini tumepata majibu ambayo hayajatupa imani. Mchezaji huyu alipata kadi nyekundu katika mechi iliyopita, lakini akacheza tena kwenye fainali,” ilielezwa katika malalamiko hayo.
Mchezo wa fainali kati ya AYE Football Academy na Greenland uliisha kwa sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 90 na kuamua mshindi kwa mikwaju ya penalti, hatua ambayo nayo imeibua malalamiko kutokana na maamuzi ya waamuzi wakati wa upigaji wa penalti.
AYE Football Academy imedai kuwa katika baadhi ya mikwaju hiyo kulikuwa na maamuzi ya utata, ikiwemo tukio ambalo kipa alidaiwa kutoka kwenye mstari kabla ya penalti kupigwa na mwamuzi kuamuru ipigwe tena, jambo ambalo academy hiyo inalipinga.
Malalamiko hayo yamefikia kwa Afisa Michezo anayetajwa kwa jina la Mwakitema, ambaye kwa mujibu wa AYE Football Academy alisema suala hilo lingepelekwa kwa mwenyekiti wa kamati ili kujadiliwa na kuangaliwa namna ya kulitatua kabla ya kutolewa kwa zawadi za mshindi.
Hata hivyo, AYE Football Academy imesema haina imani na kamati ya maandalizi kutokana na namna ambavyo imedai masuala hayo yameshughulikiwa, ikisisitiza kuwa ina ushahidi wa video na picha unaohusiana na baadhi ya matukio inayolalamikia.
“Watu wanajitahidi kupambana, kuibua vipaji na kuwekeza kwenye hizi ligi, lakini mambo kama haya yanakatisha tamaa. Tunataka kanuni zitumike kwa usawa na kama tumedhulumiwa, tupewe haki yetu,” kilisema chanzo hicho.
AYE Football Academy imeonya kuwa endapo suala hilo halitapatiwa ufumbuzi kwa kuzingatia kanuni, iko tayari kuzungumza na waandishi wa habari na kuweka hadharani ushahidi ilionao huku ikitaka kamati ya mashindano kutoa ufafanuzi wa wazi kuhusu maamuzi yaliyofanyika katika hatua mbalimbali za mashindano.